Mancini na Esposito waiokoa Italia moldova

CHISINAU: MABAO ya dakika za lala salama kutoka kwa Gianluca Mancini na Francesco Pio Esposito yaliipa timu ya taifa ya Italia ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Moldova, na kufufua matumaini ya kuendelea kusalia kwenye mbio za kutafuta nafasi ya kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia 2026.
Ushindi huu umeifanya Italia kuwa na pointi 18 katika nafasi ya pili, ikiwa nyuma ya vinara Norway kwa pointi tatu, ambao awali waliifunga Estonia mabao 4-1. Timu hizo mbili zinakutana Jumapili kwenye mchezo wa mwisho wa kufuzu, lakini Azzurri wana kazi ngumu ya kushinda mchezo na kupindua tofauti ya mabao ya 17 ya Norway, jambo linaloonekana kama haliwezekani.
Kocha wa timu hiyi Gennaro Gattuso amesema amefurahishwa na utulivu na ubora wa kikosi chake, licha ya mchezo huo kuwa mgumu kwa muda mrefu.
“Nimeiona Italia iliyocheza vizuri, Moldova hawakupiga shuti golini. Tumefanya tulichopaswa kufanya na tukawapa nafasi baadhi ya vijana.” amesema Gattuso.

Kwa zaidi ya dakika 80 Italia ilimiliki mpira lakini ikajikuta ikikwama mbele ya safu ya ulinzi imara ya Moldova. Giacomo Raspadori na Mancini walikaribia kufunga, huku Moldova wakiwa tishio mara moja tu kupitia Virgiliu Postolachi aliyepaisha mpira juu.
Mabadiliko ya kipindi cha pili yaliipa Italia nguvu mpya baada ya kuingizwa Esposito na Mateo Retegui, lakini ngome ya Moldova iliendelea kusimama imara hadi dakika ya 88, ambapo Federico Dimarco alitoa krosi safi na Mancini akapaa kupiga kichwa kilichotinga kona ya chini ya goli.
Dakika mbili baada ya muda wa nyongeza kuanza, Esposito aliongeza bao la pili kwa kichwa baada ya krosi ya Matteo Politano, akifunga bao lake la pili la kimataifa.
Gattuso alikiri mchezo ulikuwa na hatari yake, akisema, “Kwa kuwa na kikosi kipya mwanzo, nilihofia hata kama tungeweza kupoteza. Lakini nawapongeza kwa walivyocheza.”
Italia, ambayo ilishindwa kufuzu Kombe la Dunia mara mbili mfululizo (2018 na 2022), sasa inapambana kuepuka kutolewa kwa mara ya tatu mfululizo, jambo ambalo lingeongeza presha kwa taifa lenye historia kubwa ya soka. Moldova inabaki mkiani ikiwa na pointi moja na bado haijapata ushindi.




