Man U yakubali kumuuza Garnacho

MANCHESTER: CHANZO cha karibu na Mashetani wekundu Manchester United kimeliambia shirika la Habari la BBC kuwa wababe hao wamekubali kumuuza winga wao raia wa Argentina Alejandro Garnacho kwenda Chelsea kwa dau la pauni milioni 40.
Thamani ya mauzo ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 itakuwa ya nne kwa ukubwa kwa mchezaji wa United baada ya Cristiano Ronaldo, Romelu Lukaku na Angel di Maria.
Garnacho, ambaye amechezea United mechi 93 za Premier League, ni miongoni mwa wachezaji watano waliotaka kuondoka katika klabu hiyo msimu huu, akiwa pamoja na, Antony, Tyrell Malacia, Jadon Sancho na Rashford aliyejiunga na Barcelona kwa mkopo mwezi uliopita.
Meneja wa kikosi hicho Ruben Amorim amemuacha Garnacho nje ya kikosi chake msimu huu, huku United ikishindwa kushinda mechi zao mbili za kwanza za Ligi kabla ya kutupwa nje ya Kombe la Carabao kwa mikwaju ya penalti na Grimsby Town timu ya daraja la nne.