TAARIFA kuwa baba yake amebakiza muda mfupi sana wa kuishi duniani inamkuta Nick Cassidy akiwa nyuma ya nondo.
Wakati akiwa bado hajajua aipokee vipi habari hiyo, siku mbili baadaye anajikuta akifungwa pingu ili akahudhurie mazishi. Nick analia akiwa jela, na analia tena anaposimama mbele ya jeneza la baba yake.
Huyu ni askari wa zamani ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 25 ndani ya gereza la Sing Sing Correctional Facility kwa madai ya kuiba almasi ya kifalme yenye thamani ya dola milioni 40 kutoka kwa mfanyabiashara, David Englander.
Nick, hata hivyo, anaendelea kusisitiza kuwa hana hatia na anamshutumu mfanyabiashara Englander kwa kumtungia kesi ya wizi wa almasi hiyo, na hivyo, njia pekee inayomjia akilini ya kulisafisha jina lake ni kutoroka kutoka jela.
Ndiyo, Nick Cassidy anahudhuria msiba wa baba yake lakini anahakikisha kuwa harudi tena jela. Anaondokea palepale makaburini, tena mbele ya macho ya askari akiwaonesha kuwa hata yeye alikuwa askari hapo kabla.
Na hapo ukurasa unafungwa na mwingine mpya unafunguliwa. Ni katika Jiji la New York, Nick anafika na kupanga chumba katika Hoteli ya Roosevelt kwa jina bandia la Walker, anachukua chumba kwenye gorofa ya 21 na analipia, na chakula analetewa lakini hakula.
Ana jambo lake. Ni jambo hilo ndilo linalofunga mitaa ya Manhattan jijini New York. Ni kwa jambo hilo ndipo maofisa wa polisi wanapouona uwendawazimu wa mtu anayedai haki. Mwanzoni inaanza kama utani.
Watu wanadhani kuwa haiwezekani, na wengine wanaamini ni maigizo. Ndani ya chumba chake alichopanga katika ghorofa ya 21, Nick anafungua dirisha na kusimama kwenye ukingo uliobakiza sehemu ndogo tu ya kiatu chake, akiwa tayari kujiua.
Umati wa watu hapo chini ya jengo unatoa taarifa polisi juu ya uwepo wa mtu anayetaka kujiua kwa kujirusha ghorofani. Maofisa wa polisi wanafika hotelini hapo na kuanza uchunguzi.
Dante Marcus anajaribu kudhibiti umati wa watu, wakati Jack Dougherty anajaribu kuzungumza na Nick. Walakini, Nick hataki kuongea na mtu yoyote kati yao, isipokuwa mwanamke mmoja tu!
Wanashangaa, yaani mwanamke ndiyo amsimamishe mwanamume huyo hapo na kuufanya mji mzima usimame kwa saa kadhaa! Yaani ni mwanamke tu ndiyo anafanya nchi itangaze ‘mbashara’ habari yake! Huu ni mpango kabambe! Nick anasisitiza kuwa asipoletewa anachokitaka atajirusha toka ghorofani.
Kutaka kujiua ni kosa kubwa kisheria, na Nick analijua hilo ndiyo maana yupo hapo kwa makusudi. Anavunja sheria anayoijua! Hata hivyo, nyuma ya tukio la Nick kuna uhalifu unaotakiwa kudhibitiwa.
Polisi hawawezi kusogea aliposimama Nick, ni sehemu hatari sana. Njia pekee ni kumtimizia mahitaji yake. Anaulizwa ni mwanamke gani anayemtaka, Nick anawajibu, “Lydia Mercer”.
Nick atazungumza tu na Lydia, ambaye yuko likizo, baada ya kushindwa kuokoa maisha ya polisi aliyejiua kwenye Daraja la Brooklyn. Kwa kawaida Lydia ana kazi moja tu ndani ya jeshi la polisi.
Kila anapohitajika mtu wa kushawishiwa jambo fulani gumu, basi huitwa mwanamke huyu. Nick anawatuma polisi wamuitie Lydia kwani ndiye anayeweza kumshawishi ashuke pale. Polisi wanashangaa! Mbona hajirushi kama kweli ni mtu anayetaka kujirusha!
Inaonesha kuwa anawasumbua. Baada ya muda Lydia anafika kwenye chumba cha hoteli na anafanya kila uwezo wake kuongea na Nick ili atoke pale kwenye ukingo wa jengo. Anamuhakikishia usalama wake baada ya tukio lile.
Asichokijua Lydia na jeshi lote la polisi ni kitu kimoja tu, Nick hayupo pale kwa bahati mbaya. Huo ni mpango mkakati uliotokana na akili iliyopangwa mwaka mmoja nyuma. Nick anauhitaji muda wa polisi.
Anataka ‘attention’ ya nchi yote ya Marekani iwe kwake. Na ndicho kinachotokea sasa. Lengo lake ni moja tu, ile almasi aliyosingiziwa kuwa kaiiba mpaka akafungwa jela, sasa anataka kuiiba kweli!
Wasichokijua polisi, Nick anawasumbua tu wakati huo kaka yake, Joey na rafiki wa kike wa Joey, Angie, wanaingia ndani ya duka la vito vya mapambo katika chumba cha Englander, upande wa pili wa mtaa, wakitumia muda ambao Nick anawafanyia maigizo polisi kulipua juu ya paa na kuingia iliwaibe almasi na mwishowe ithibitishwe kuwa Nick hana hatia.
Muda wote maofisa wa polisi wana heka heka za kufunga mitaa na zimamoto wa mji mzima wanarundikana pale hotelini. Wakati huo Joey na Angie wanafanya yao ndani ya chumba cha Englander.
Nick anatumia mbinu ya hali ya juu kuwasiliana na kina Joey kwa kutumia mikrofoni ndogo za kunasa sauti huku akiendelea kuwapumbaza maofisa wa polisi kuwa anataka kujirusha. Ni suala la kuununua muda wa jeshi la polisi kwa gharama ya kuwapigisha stori!
Polisi wanajitahidi kumshawishi Nick asijirushe toka ghorofani, kumbe kina Joey wanafanya tukio kubwa. Nick anaonesha jinsi alivyo na akili nyingi kuwazidi polisi na anataka kuionesha dunia matumizi sahihi ya akili.
Wanapotambua kuwa mwanamume anayetaka kujirusha ni Nick Cassidy, Marcus anaamuru polisi waweke usalama kwenye duka la vito vya mapambo na kwenye chumba cha Englander.
Muda ambao polisi wanagundua kuwa wameibiwa akili wanajiona kuwa hawakuwa nazo hata hizo akili zenyewe! Yote haya utayapata ndani ya filamu ya Man on a ledge inayosisimua, iliyotoka mwaka 2012 nchini Marekani, ikiongozwa na Asger Leth.
Kwa asilimia kubwa upigaji picha za filamu ulifanyika juu ya Hoteli ya Roosevelt jijini New York. Ilipotoka ilikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wakosoaji wa filamu na iliingiza dola milioni 8 (ndani ya Marekani) katika wiki yake ya ufunguzi.




