
UONGOZI wa timu ya Ruvu Shooting umemtangaza Mbwana Makata kuwa kocha mpya wa timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja akichukua mikoba iliyoachwa wazi na Charles Mkwasa aliyeamua kuacha kazi.
Mkwasa amejiuzulu nafasi hiyo Desemba 5 kutokana na mwenendo mbaya wa Ruvu Shooting katika Ligi Kuu Tanzania bara.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Ofisa habari wa timu hiyo Masau Bwire amesema Ruvu imemchagua Makata sababu inafahamu uwezo wake na ina imani atabadili mwenendo wa timu.
“Tunamshukuru Mkwasa kwa kazi nzuri na tunamtakia maisha mema huko anakokwenda katika maisha yake ya mpira lakini pia tunamkaribisha Makata imani yetu atatupa mafanikio katika kipindi cha mwaka huo mmoja atakaokuwa na sisi,” amesema Bwire.
Kiongozi huyo amesema malengo ni kuhakikisha Ruvu Shooting inafanya vizuri hivyo kuna mpango wa kufanya usajili kwenye dirisha dogo ili kurudi timu kwenye ushindani.
Ruvu Shooting kwa sasa inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa lig ikiwa na pointi 11 baada ya michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.