Madrid yairahisishia Arsenal usajili

LONDON, Meneja wa Washika mitutu wa jiji la London Arsenal Mikel Arteta, amesema ushindi mkubwa walioupata dhidi ya Real Madrid ushindi uliowapeleka katika nusu fainali yao ya kwanza ya Champions League tangu 2009, utachochea nguvu yao ya kusaka majina makubwa katika dirisha la usajili lijalo.
Arteta amekuwa na dhamira ya kusajili mshambuliaji tangu Januari japo nyota wake Mikel Merino amekuwa na mwenendo unaomridhisha Kocha huyo. Majina kadhaa yamehusishwa na Arsenal akiwemo mchezaji wa Sporting Lisbon Viktor Gyokeres, Benjamin Sesko wa RB Leipzig na nyota wa Athletic Bilbao Nico Williams.
“Huenda tumepata sababu mpya, lakini mara zote tumekuwa na bahati kwa sababu sisi ni klabu ambayo kila tukifanya mazungumzo na mchezaji anakuwa tayari kujiunga nasi”
“Lakini hii itachochea zaidi imani nasi na wachezaji sasa watasema ‘nataka kuwa sehemu ya usiku wa Ulaya’ kwa sababu sasa klabu yetu iko katika nafasi nzuri, kiujumla kwa sasa sisi ni vigogo tunaweza kumvutia mchezaji yeyote” – Arteta aliwaambia waandishi wa habari
Arteta pia amegusia uwezekano wa mshambuliaji wake Mjerumani Kai Havertz kurejea msimu huu akisema kuwa huenda asiwe fiti kucheza nusu fainali lakini kwa maendeleo aliyonayo anaweza kurejea kabla ya msimu huu kumalizika.
Arsenal waliiondoa Real Madrid kwa kipigo cha aibu cha jumla ya mabao 5-1 wakishinda michezo yote ya robo fainali ya UEFA Champions League na sasa watakutana na vigogo wa Ufaransa Paris St Germain (PSG) April 29.