Liverpool yamponza Maresca, afungiwa mechi moja

LONDON: KOCHA mkuu wa mabingwa wa Dunia Chelsea, Enzo Maresca, amefungiwa mechi moja na kutozwa faini ya pauni 8,000 baada ya kukiri kosa la utovu wa nidhamu (improper conduct) katika ushindi wao wa mabao 2–1 dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool kwenye Ligi Kuu ya England wiki iliyopita.
Tukio hilo lilitokea uwanjani Stamford Bridge, baada ya kinda wa Brazil Estêvão Willian kufunga bao la ushindi la dakika za jioni lililoibua shangwe kubwa. Maresca, akiwa tayari amepewa kadi ya njano awali, alikimbia kuelekea wachezaji wake kushangilia nao jambo lililomfanya mwamuzi wa mchezo huo Anthony Taylor kumpa kadi ya pili ya njano kisha nyekundu na kumtoa nje ya eneo la benchi la ufundi.
Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka la England (FA), imeelezwa kuwa Maresca alikubali makosa yake na kukubali kupokea adhabu hiyo bila kukata rufaa.
“Kocha Enzo Maresca amekiri kosa la kuonesha tabia isiyofaa na ameadhibiwa kwa mujibu wa kanuni za FA,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya shirikisho hilo.
Adhabu hiyo inamaanisha kuwa Maresca hatakalia benchi la ufundi wakati Chelsea watakapovaana na Nottingham Forest wikendi hii. Huku Msaidizi wake, Willy Caballero, akitarajiwa kuchukua majukumu ya kusimamia timu hiyo katika mchezo huo.
Hii ni mara ya pili kwa Maresca kupewa adhabu kwa utovu wa nidhamu tangu aanze kazi yake Stamford Bridge, jambo linalozua maswali kuhusu uwezo wake wa kudhibiti hisia katika mazingira ya ushindani mkali.