Licha ya kutocheza msimu huu, Bissouma Mali

BAMAKO: KOCHA wa timu ya taifa ya Mali amemjumuisha kiungo wa taifa hilo Yves Bissouma kwenye kikosi cha kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) licha ya kutokucheza mechi yoyote ya klabu msimu huu, hatua iliyoibua mjadala lakini pia kuonesha kiwango cha imani aliyojengewa na benchi la ufundi.
Kocha Tom Saintfiet alimtaja Bissouma mwenye umri wa 29, katika kikosi la wachezaji 28 watakaoiwakilisha Mali kwenye fainali zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21. Hii ni licha ya kiungo huyo wa Tottenham Hotspur kutoshuka dimbani tangu mwezi Agosti.

Bissouma aliondolewa kwenye kikosi kabla ya mchezo wa Super Cup dhidi ya Paris Saint-Germain, na baadaye akafanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu kufuatia jeraha alilopata kwenye mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia. Tangu wakati huo hajarejea dimbani.
Licha ya hali hiyo, Saintfiet ameonesha msimamo kwamba uzoefu na ubora wa Bissouma vinabaki kuwa muhimu kwa timu hiyo ya taifa, hususan kwenye mashindano makubwa kama AFCON.
Mali wataanza kampeni yao ya Kundi A dhidi ya Zambia Desemba 22 jijini Casablanca, kabla ya kukutana na wenyeji Morocco na kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya Comoros.




