Lady Jay Dee kupamba usiku wa Valentine

DAR ES SALAAM: MSANII nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura maarufu kama Lady Jay Dee, anatarajiwa kupamba na kunogesha Usiku wa Wapendanao (Valentine’s Day) katika ukumbi wa Brake Point, Makumbusho jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Lady Jay Dee amesema anafahamu jinsi Watanzania wanavyompenda na amewaahidi burudani ya hali ya juu itakayogusa hisia za wengi, hasa katika siku hiyo maalum ya mapenzi.
“Nawajua Watanzania wananipenda, na wategemee burudani nzuri na ya kipekee kutoka kwangu,” amesema Jay Dee.
Aidha,amewahamasisha mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo, akisisitiza kuwa mtu anaweza kuchagua kuja peke yake bila kusubiri mwaliko kutoka kwa mwingine.
“Chagua kuja mwenyewe Brake Point Makumbusho bila kusubiri mtu. Lakini pia chagua nani wa kumpenda na kuja naye. Chagua unachoamua kuchagua bila kuchaguliwa,” amesisitiza.
Katika kuongeza hamasa ya usiku huo, Lady Jay Dee ametangaza ofa maalum kwa wapenzi watakaovishana pete katika tukio hilo.
Amesema atatoa zawadi ya kuwaimbia bure katika harusi yao, mradi harusi hiyo ifanyike kati ya mwezi Mei hadi mwisho wa Septemba mwaka huu.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwa la kipekee, likiwakutanisha wapenzi na mashabiki wa muziki katika kusherehekea siku ya mapenzi kwa burudani safi kutoka kwa malkia huyo wa Bongo Fleva.




