Michezo Mingine

Kriketi yaendelea kuitangaza Tanzania kimataifa

DAR ES SALAAM:KATIBU  Mtendaji Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, amesema mafanikio makubwa ya Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) yamekuwa chachu ya timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 19 kufuzu kushiriki Kombe la Dunia litakalofanyika Februari 2026 nchini Zimbabwe.

Msitha aliyasema hayo alipomwakilisha Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kriketi Afrika unaofanyika katika Hoteli ya White Sands, jijini Dar es Salaam.

“Juhudi, uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) vimekuwa kivutio na kishawishi si tu hapa nchini bali pia barani Afrika,” amesema.

Msitha amehakikishia viongozi wa kriketi Afrika na Dunia kuwa Tanzania ni sehemu salama, yenye amani na vivutio vingi vya kiutalii, na kuwasihi wasisite kuja kuandaa mikutano yao nchini humo, akisisitiza kuwa hawatajuta kufanya hivyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Kriketi Duniani (ICC), Mubashshir Usman, amesema  mikakati yao inalenga kuhakikisha mchezo wa kriketi Afrika unapiga hatua kubwa tofauti na hali iliyokuwepo miaka ya nyuma.

Mkutano huo wa siku tatu jijini Dar es Salaam umetajwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili maendeleo ya wachezaji wa Afrika katika mashindano ya Dunia pamoja na kupanga mikakati mipya ya kuendeleza mchezo huo barani humo.

Related Articles

Back to top button