Kompany akerwa na jeraha la Musiala

ATLANTA, Meneja wa Bayern Munich Vincent Kompany amesema alikasirika baada ya Jamal Musiala kupata jeraha la kutisha wakati wa kipindi cha kwanza cha mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Paris St Germain mjini Atlanta Jumamosi.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 22 alipata majeraha kwenye dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza cha mchezo huo kufuatia kugongana na golikipa Donnarumma kwenye eneo la hatari la PSG.
Musiala alikuwa akimpiga chenga beki wa PSG William Pacho kabla ya kipa Gianluigi Donnarumma bila kukusudia kukilalia kifundo cha mguu wa kushoto cha Musiala na kuuzungusha kwa namna ya kutisha na kumwacha akiwa amelala akiugulia maumivu uwanjani.
“Ni mara chache sana nimekuwa na hasira wakati wa mapumziko, sio dhidi ya wachezaji wangu. Kuna mambo mengi maishani ambayo ni muhimu, muhimu zaidi kuliko haya. Lakini mwisho wa siku kwa wachezaji haya ni maisha yao. Na mtu kama Jamal haya ni maisha yake ukizingatia ametoka kwenye majeraha mengine alafu linatokea hili kwa jinsi linavyotokea kwakweli nakosa nguvu”
“Ninapokaa hapa karibu nanyi, kitu kinachofanya damu yangu inachemka muda huu sio matokeo, naelewa huu ndo mpira wa miguu, lakini ni kweli kwamba ilitokea kwa mtu ambaye anafurahia sana kucheza lakini pia ni muhimu sana kwetu.” – Kompany aliwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo.




