Ligi KuuNyumbani

Kombe jipya Ligi Kuu hili hapa

WAKATI kila timu ikiwa imesaliwa na mchezo mmoja kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la Ligi Kuu Tanzania bara kwa msimuu huu, maandalalizi ya kuufunga msimu yamepamba moto.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo imetambulisha kombe jipya kwa ajili ya ligi hiyo ambalo litakuwa la kudumu ili kuwa nembo ya utambulisho kwa ligi.

Mwakilishi wa TPLB Ibrahim Mwayela amesema Bodi ilipokea mapendekezo ya wadau mbalimbali  juu ya maboresho ya muenekano wa kombe hilo mara baada ya kulitambulisha msimu uliopita.

“Msimu uliopita tulipata maoni mbalimbali, na sisi tuliyapokea na kuyafanyia kazi, tunaendelea kuyapokea na kujifunza, kama mnavyofahamu ligi yetu inashika nafasi ya tano kwa ubora Afrika kwa hiyo ni lazima kombe liendane na ubora wa ligi,” Amesema Mwayela.

Kwa upande wa mwakilishi wa mdhamini mkuu wa ligi benki ya NBC Godwin Semunyu amesema nia ni kuwa na kombe bora ili kuipa hadhi zaidi ligi hiyo.

“Ni kombe ambalo limetengenezwa kutoka Afrika kusini, lengo la NBC ni kutaka ligi kuu iendelee kuwa bora,” amesema Semunyu.

Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2022/23 watakuwa wa kwanza kukabidhiwa kombe hilo Juni 9 jijini Mbeya baada ya mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons.

Related Articles

Back to top button