EPL

Kocha mpya wa Spurs aacha moyo Brentford

LONDON, Kocha mpya wa Tottenham Hotspur Thomas Frank amesema klabu yake ya zamani Brentford, mashabiki na uongozi, na jamii inayozunguka wana sehemu kubwa ndani ya moyo wake baada ya kukubali kubeba jukumu kubwa la kufufua hali njema ya Tottenham kwenye ligi kuu ya England na mashindano mengine kwa msimu ujao.

Katika ujumbe uliojaa hisia uliochapishwa kwenye tovuti ya Brentford Frank amesema: “Muda wa mimi kuendelea na mambo mengine umefika. Lakini, hata ninapoondoka klabuni hapa, najua nimeacha sehemu kubwa ya moyo wangu, si tu kwenye klabu bali kwa jamii na bila shaka, mashabiki waaminifu na uongozi”.

“Natoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa klabu kwa kunipa nafasi ya kutimiza ndoto zangu na kwa kila mtu aliyehusika kuifanya safari yangu hapa kuwa ya kukumbukwa. Chochote tulichofanikiwa tumefanikiwa kwa pamoja, na mafanikio yetu yamejengwa na umoja, moyo, ujasiri na matamanio katika kila ngazi ya klabu na miongoni mwa mashabiki,” – aliendelea.

“Kila mtu amechangia, ninathamini mchango wa kila mtu kwa sababu kwa udogo au ukubwa kila mchango ni wa thamani sana. Sio tu naondoka katika klabu ya soka, bali nawaaga marafiki wazuri walionisapoti katika nyakati nzuri na mbaya, nitaendelea kuwa nao daima.”

Frank mwenye miaka 51 ameshinda mechi 136 kati ya 317 katika kipindi cha miaka saba aliyodumu ndani Brentford akifanikiwa kuipandisha Daraja hadi EPL mwaka 2021. Na anakuwa kocha wa nne kuifundisha Tottenham tangu 2021, huku akiwa na jukumu la kuiinua klabu hiyo kuirejesha ndani ya kundi la klabu kubwa za Premier League.

Related Articles

Back to top button