
KOCHA Msaidizi wa Coastal Union, Joseph Lazaro ameshauri klabu za mpira wa miguu nchini kuongozwa na watu wenye taaluma ya mchezo huo vinginevyo soka la Tanzania litazidi kudidimia.
Lazaro amesema hayo alipozungumza na SpotiLeo baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Yanga kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Disemba 20.
Amesema Coastal kufungwa na Yanga kumetokana na viongozi kutokuwa na taaluma ya kutosha ya mchezo wa soka baada ya kumfukuza Kocha Mkuu Yusuf Chipo siku moja kabla ya mchezo.

“Mnamfukuzaje kocha siku moja kabla ya mchezo tena bila sababu za msingi. Hili limewavunja moyo wachezaji sababu hatujui wengine walikuwa na mapenzi naye kiasi gani,” amesema Lazaro.
Amesema kitendo hicho kinapaswa kuwa fundisho kwa klabu nyingine ambazo zinapaswa kuajiri watu wenye uelewa mzuri wa mchezo huo ili kuepuka mambo kama hayo kujitokeza.