Muziki

Kim Kayndo asema Muziki wa bongo hauthaminiwi,

atoa sababu show ya Davido

DAR ES SALAAM:MENEJA wa msanii Zuhura Othman ‘Zuchu’, anayefahamika kwa jina la Kim Kayndo, amesema kuwa muziki wa Bongo haupati thamani inayostahili kutoka kwa Watanzania wenyewe, hali inayowakatisha tamaa wasanii wa ndani.

Kauli hiyo ameitoa baada ya kuonyesha kutoridhishwa na mijadala ya vyombo vya habari pamoja na mashabiki kufuatia onyesho la msanii wa Nigeria, Davido, lililofanyika nchini Tanzania, akisema mjadala huo unaakisi namna muziki wa ndani unavyopuuzwa.

Kupitia Instagram Story yake, Kim Kayndo amesema hali hiyo inaonesha wazi kuwa juhudi za wasanii wa Tanzania pamoja na muziki wao havithaminiwi ipasavyo katika soko la ndani.

Kwa mujibu wake, kwa zaidi ya miaka 10, soko la Tanzania limekuwa likichangia chini ya asilimia 30 ya mapato ya wasanii, jambo linalowalazimu wengi kujipanga kimataifa badala ya kutegemea soko la nyumbani.

Ameeleza kuwa hali hiyo husababisha wasanii kushindwa kuwekeza vya kutosha katika kazi zao, kukosekana kwa nyimbo zenye ubora wa juu, pamoja na wengi wao kuendelea kukumbwa na changamoto za kifedha.

Aidha, Kim Kayndo amekosoa mambo kadhaa yanayokwamisha ukuaji wa muziki wa Bongo, ikiwemo ukosefu wa booking agencies imara, wasanii kulipwa chini ya thamani ya brand zao, vyombo vya habari kuibua mashindano na migogoro isiyo na tija, pamoja na DJs wa ndani kupiga muziki wa nje kwa wingi kuliko wa nyumbani.

Kauli ya Kim Kayndo imezua mjadala mpana mitandaoni, ambapo wadau wa muziki wameendelea kutoa maoni kuhusu mustakabali wa muziki wa Tanzania na wajibu wa kila mdau katika kuukuza.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button