Kila mtu ashinde mechi zake

MWANZA: KIKOSI cha Yanga kimeendelea kuonesha ubabe wake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Yanga ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 28 kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Chadrack Boka.
Stephanie Aziz Ki aliongeza mabao mawili kwa Yanga, akifunga dakika ya 75 na 77. Bao la pili lilitokana na pasi safi ya Max Nzengeli, kufuatia kazi nzuri ya Jonathan Ikangalombo, aliyeingia kuchukua nafasi ya Clement Mzize.
Kocha wa Yanga, Hamdi Miloud, alifanya mabadiliko kwa kumuingiza Jonathan Ikangalombo, ambaye hii ilikuwa mechi yake ya kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo wakati wa dirisha dogo la usajili.
Kwa ushindi huo, Yanga inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 58, ikiwa na tofauti ya alama saba dhidi ya mpinzani wake Simba SC, ambaye ana pointi 51 na michezo miwili mkononi.