Ligi Kuu

Kijili afunguka baada ya kusepa Simba

DAR ES SALAAM: BEKI mpya wa Singida Black Stars, Kelvin Kijili, ameweka wazi dhamira yake ya kupambana kwa ajili ya mafanikio ya klabu hiyo, mara baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea Simba.

Singida Black Stars imemtangaza rasmi Kijili kuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya kimataifa ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika, hatua inayodhihirisha mikakati ya klabu hiyo kujenga kikosi imara.

Akizungumza baada ya kutambulishwa, Kijili amesema anauchukulia uhamisho wake kama ukurasa mpya wa maisha yake ya soka na kwamba yupo tayari kuonesha uwezo wake uwanjani kwa ajili ya kulinda heshima ya timu hiyo.

“Kwa sasa ni mchezaji halali wa Singida Black Stars. Huu ni mwanzo mpya kwangu na nipo tayari kushirikiana na wachezaji wenzangu kupambania nembo ya klabu hii kwenye mashindano yote,” amesema beki huyo mahiri.

Kijili ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Singida Black Stars, huku akileta uzoefu mkubwa alioupata akiwa na miamba ya soka nchini, Simba.

Kwa sasa, Singida Black Stars inaendelea na mikakati ya usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kikuu pamoja na timu ya pili ambayo pia itashiriki mashindano mbalimbali kwa lengo la kuongeza ushindani ndani ya klabu.

Usajili wa Kijili unatazamwa kama hatua muhimu kwa Singida Black Stars, inayojipanga kwa msimu wenye ushindani mkubwa ndani na nje ya nchi.

Related Articles

Back to top button