Kifo cha Jota: Wadau wa soka wamiminika msibani

GONDOMAR, Viongozi na Wachezaji wa Liverpool ni miongoni mwa waliokusanyika katika mji mdogo wa Gondomar nchini Ureno mapema leo Jumamosi kwa mazishi ya mchezaji mwenzao wa Ligi Kuu ya England Diogo Jota, aliyefariki akiwa na mdogo wake katika ajali ya gari nchini Hispania siku ya Alhamisi.
Nahodha wa Liverpool Virgil Van Dijk, mlinda mlango Caoimhin Kelleher na meneja Arne Slot walikuwa miongoni mwa wachezaji wenzake wa zamani na wa sasa waliofika Ureno Ijumaa jioni kutoa heshima zao za mwisho kwa mshambuliaji huyo na mdogo wake Andre Silva.
Wadau wengine pia wanatarajiwa kuungana na familia inayoomboleza na mamia ya wakazi wa Gondomar, mji mdogo kaskazini mwa Ureno ambako Jota alikulia, kwa ajili ya mazishi katika kanisa la Igreja Matriz.
Mwanadada Rute Cardoso, ambaye alifunga ndoa na Jota wiki chache zilizopita, anatarajiwa kuongozana na watoto watatu wadogo wa wanandoa hao.
Kifo cha Jota katika umri wa miaka 28 kimeleta mshtuko mkubwa katika ulimwengu wa soka na kwingineko, huku jumbe za rambirambi zikimiminika kutoka kwa viongozi wa kitaifa na pia katika michezo mbalimbali.