Muziki

Khaligraph Jones kutumbuiza baada ya mechi za HSBC SVNS 2 Nyayo Stadium

NAIROBI: MSISIMKO wa burudani katika mashindano ya raga ya HSBC SVNS 2 Nairobi umeendelea kupanda baada ya waandaaji kuthibitisha rasmi kuwa mastaa wakubwa wa muziki wa Kenya, Khaligraph Jones na Vijana Barubaru, wataongoza sherehe za burudani za baada ya mechi (afterparty) zitakazofanyika katika Uwanja wa Nyayo.

Burudani hiyo ya siku mbili inawezeshwa na kampuni ya Tusker, ambayo imedhamini mashindano hayo kwa kiasi cha Shilingi milioni 40 za Kenya, hatua inayodhihirisha dhamira ya chapa hiyo katika kuboresha uzoefu wa mashabiki na kuunga mkono maendeleo ya mchezo wa raga nchini Kenya.
Mashabiki wanatarajiwa kushuhudia burudani ya aina yake kutoka kwa Khaligraph Jones, mmoja wa wasanii wakubwa na wenye ushawishi mkubwa katika muziki wa hip hop Afrika Mashariki.

Msanii huyo anayejulikana kwa uwezo wake mkubwa wa kutawala jukwaa anatarajiwa kuwapeleka mashabiki katika safari ya muziki kupitia nyimbo zake maarufu kama Mazishi, Yes Bana na Yego, pamoja na kazi zake mpya zikiwemo Uspimee, WeYuAt, Confused na Nature Ya Binadamu.

Atasaidiwa na ma-DJ kadhaa maarufu akiwemo DJ Tophaz, DJ Daffy, DJ Deewiz na DJ Confy, huku MC Gogo na MC maarufu wa raga Azuu wakitarajiwa kudumisha hamasa kabla na baada ya burudani, kuhakikisha hali ya shangwe inatawala usiku mzima.

Related Articles

Back to top button