Kwingineko

Kesi ya milioni 6 za Kenya yamfilisi Black Cinderella

NAIROBI: MWANAMTANDAO maarufu kutoka nchini Kenya, Maureen Imbayi, maarufu kwa jina la Black Cinderella, amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa kesi ya madai ya kudhalilisha (defamation) dhidi ya mtangazaji maarufu wa Kenya, Oga Obinna, ambapo aliamriwa kulipa fidia ya jumla ya Shilingi milioni sita.

Kupitia video aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa TikTok, Black Cinderella alionekana kutokujali hukumu hiyo, akisema kuwa hana mpango wa kulipa fidia hiyo bali atachukua hatua ya kutangaza kufilisika (bankruptcy).

“Mbona nikimbie? Nitasimama, nilipie, na nimwambie Mheshimiwa Jaji, ‘hii ndiyo hali yangu.’ Nitatangaza kufilisika. Sina kitu, sina mali, sina payslip, sijawahi kuajiriwa,” alisema kwa ujasiri.

TikToker huyo ambaye amejizolea umaarufu kupitia video zake za utani na mahojiano ya mtandaoni kama “jaji wa mahakama ya mtandaoni”, alikiri wazi kuwa amekuwa akijihusisha na shughuli zisizo za maadili ili kujikimu kimaisha, akisisitiza kuwa kipato chake kidogo hakiwezi kufidia kiasi hicho kikubwa cha pesa.

“Sina mali yoyote ya kuuza au kumtumia hizo pesa. Sina hicho kiwango cha pesa,” aliongeza kwa msisitizo.

Kesi hiyo ilianzia mwaka 2023 baada ya mahojiano kwenye kipindi cha Massawe Japanni kupitia Radio Jambo, ambapo Black Cinderella alitoa kauli kadhaa za kumdhalilisha Obinna.

Obinna alikanusha madai hayo hadharani, akisema hajawahi hata kukutana na Black Cinderella. Baada ya hapo, aliamua kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya Cinderella, Massawe Japanni na Radio Jambo, akidai kauli hizo ziliharibu taswira yake, kazi na chapa (brand) yake.

Baada ya miezi kadhaa ya mvutano wa kisheria, mahakama hatimaye ilitoa uamuzi kwa niaba ya Obinna, na kuthibitisha kuwa alidhalilishwa hadharani.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Obinna alisherehekea ushindi huo akisema:
“Tulifungua kesi ya madai ya kudhalilisha dhidi ya Massawe Japanni, Black Cinderella, na Radio Jambo mwaka jana na leo tumeshinda. Jina langu lilibomolewa, heshima yangu ikaharibiwa, na hawakuwahi kuomba radhi. Sasa haki imetendeka.”

Kulingana na uamuzi wa mahakama, washtakiwa walitakiwa kulipa jumla ya Sh6 milioni, ikiwemo:
Sh5 milioni kama fidia ya jumla, Sh500,000 kama fidia ya adhabu (aggravated damages), Sh500,000 kwa niaba ya kuomba radhi, na Sh100,000 kama fidia ya mfano (exemplary damages).

Mahakama pia ilitoa amri ya kudumu inayowazuia washtakiwa hao kutoa tena au kusambaza kauli zozote zinazomdhalilisha Obinna katika siku zijazo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button