Kasililika kufungua michuano ya Dunia leo

DUBAI: MASHINDANO ya Ubingwa wa Dunia ya Chama cha Kimataifa cha Ngumi (IBA) yanaanza rasmi leo jijini Dubai, Falme za Kiarabu ambapo Bondia wa Timu ya Taifa ya Tanzania “Faru Weusi”, Enzi Kasililika, atafungua pazia kwa kwa kupanda ulingoni dhidi ya Joshua Cousin wa Shelisheli.
Pambano la Kasililika litakuwa katika uzani wa kilo 75 (Middleweight), likiwa pambano la 37 litakalopigwa kuanzia saa 2:00 usiku (muda wa Tanzania) katika Uwanja wa Tennis wa Dubai Duty Free.
Jumla ya mataifa 108 yanashiriki mashindano haya ya wanaume katika uzani 13 tofauti.
Mashindano haya makubwa yanatoa zawadi za kihistoria zenye jumla ya Dola za Kimarekani milioni 8.32 (takribani Bilioni 20.8) ambapo washindi watapata zawadi kama ifuatavyo kuanzia mshindi wa kwanza mpaka wa tano.
1. USD 300,000 (TZS 750,000,000)
2. USD 150,000 (TZS 375,000,000)
3 & 4. USD 75,000 (TZS 187,500,000)
5th. USD 10,000 (TZS 25,000,000)
Mgawanyo wa zawadi: asilimia 50% kwa mchezaji, 25% Shirikisho, 25% Walimu.
Katika mashindano haya, Tanzania ‘Faru Weusi’ inawakilishwa na wachezaji watano wanaochipukia, wakiongozwa na Mwalimu Mkuu Samwel Kapungu “Batman”, kama ifuatavyo:
Enzi Kasililika –kg 75 (Middleweight), Rashidi Mrema – kg 60 (Lightweight), Faki Faki kg 54 (Bantamweight), Juma Athumani kg 51 (Flyweight), Ally Ngwando kg 48 (Minimumweight)




