Kanye West kulipa fidia ya Sh18 milioni

LOS ANGELES: MAHAKAMA ya majaji jijini Los Angeles imemuamuru rapa maarufu Kanye West kulipa fidia ya takribani shilingi milioni 18 kwa aliyekuwa meneja wa mradi wake, Tony Saxon, kufuatia mgogoro wa kazi katika nyumba ya kifahari ya rapa huyo iliyopo Malibu.
Kesi hiyo ilihusisha madai ya kutolipwa mishahara, mazingira hatarishi ya kazi na kufukuzwa kazi kinyume cha sheria.
Saxon alidai kuwa alipata majeraha wakati akifanya kazi katika nyumba ya West yenye thamani ya mabilioni ya shilingi, huku akilazimika kuishi katika mazingira duni ndani ya eneo hilo.
Awali aliiomba mahakama imlipe fidia ya takribani shilingi milioni 219, lakini majaji waliamua kumpa fidia ya shilingi milioni 18 pekee bila adhabu nyingine ya ziada.
Kwa upande wake, timu ya utetezi ya West ilidai kuwa Saxon hakuwa mkandarasi mwenye leseni halali na kwamba aliharibu muundo wa nyumba hiyo.




