Kamwe: Tunajifunza kwa wakubwa ili kuvuka kundi

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema kuwa licha ya timu hiyo kufanikiwa kutimiza lengo lake la awali la kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, safari bado haijakamilika kwani wanatamani kufika mbali zaidi.
Kamwe amesema Yanga ina alama nne, ambazo bado hazitoshi kuwapa uhakika wa kufuzu hatua ya robo fainali, hivyo wanahitaji kuongeza juhudi kwenye michezo ijayo.
“Malengo yetu yalikuwa kufika hatua ya makundi ambayo tayari tumefika. Tunaangalia uwezekano wa kufika hatua inayofuata, tuna alama 4 ila hazitupi uhakika wa kufika robo fainali,” alisema Kamwe.
Amesisitiza kuwa Yanga bado inaendelea kujifunza kutokana na ugumu wa kundi walilopo, pamoja na uzoefu wa timu kubwa wanazokutana nazo.
“Bado tunaendelea kujifunza, tuko kwenye kundi gumu. Tunaendelea kujifunza kwa wakubwa namna gani tunaweza kuwa bora zaidi na kuingia robo fainali,” aliongeza.
Yanga sasa inaelekeza nguvu kwenye mechi zijazo, ikihitaji kupata pointi muhimu zitakazoamua hatma ya safari yao ya kimataifa.




