Serie A

Juventus waingia 18 za UEFA

TURIN: KLABU ya Juventus imeingia matatani baada ya Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA kuanzisha uchunguzi rasmi juu ya uwezekano wa klabu hiyo kukiuka kanuni za fedha za ‘Financial Fair Play’ (FFP), huku ripoti za kifedha zikionesha hasara kubwa na mabadiliko ya uongozi yakitarajiwa ndani ya siku chache zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na vyanzo vya ndani ya klabu, UEFA imeanzisha uchunguzi dhidi ya Juventus kutokana na mashaka juu ya uvunjaji wa kanuni za mapato ya klabu (Football Earnings Rule) kwa kipindi cha kati ya mwaka 2022 hadi 2025. Kanuni hizo zinazuia klabu kupata hasara ya zaidi ya euro milioni 60 katika kipindi cha miaka mitatu.

Ripoti za hivi karibuni zinaonesha kuwa Juventus ilipata hasara ya takriban euro milioni 58 kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025 kiwango kinachoiweka klabu hiyo kwenye hatari ya kukaribia ukomo wa hasara unaoruhusiwa na UEFA. Uamuzi wa mwisho kuhusu hatma yao unatarajiwa kutolewa mwakani.

Wakati huo huo, hali ya sintofahamu imeongezeka ndani ya menejimenti ya klabu hiyo baada ya Mkurugenzi Mtendaji Maurizio Scanavino, kutangaza kujiuzulu ifikapo tarehe 7 Novemba mwaka huu. Huku nafasi yake ikitarajiwa kuchukuliwa na Damien Comolli, ambaye kwa sasa ni Meneja Mkuu wa klabu.

Mabadiliko hayo ya uongozi yanakuja wakati ambao Juventus inakabiliana na upungufu wa mapato na mashinikizo kutoka kwa wadau wa ndani na nje ya klabu.

Hii si mara ya kwanza kwa Juventus kujikuta katika mgogoro wa kifedha. Mwaka 2023, klabu hiyo ilifungiwa kushiriki michuano ya Ulaya kwa msimu mmoja kutokana na ukiukaji wa kanuni hizo hizo za FFP, sambamba na kesi za hesabu za uongo zilizowahusisha viongozi wa zamani akiwemo Andrea Agnelli na Pavel Nedved.

Iwapo UEFA itabaini ukiukwaji mpya, Juventus inaweza kukabiliwa na adhabu kali zaidi, ikiwemo kupigwa faini, kupunguziwa nafasi za usajili wa wachezaji katika michuano ya Ulaya, au hata kufungiwa ushiriki.

Related Articles

Back to top button