Nahimana: Penati ya Jean Charles Ahoua ilikuwa kazi kubwa

DAR ES SALAAM: KIPA namba moja wa Namungo FC, Jonathan Nahimana, amesema penati iliyopigwa na mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua, ilikuwa changamoto kubwa kwake.
Nahimana ameendelea kung’ara langoni, akifanikiwa kuokoa penati mbili katika michezo miwili tofauti ndani ya wiki moja. Alicheza penati ya Leonel Ateba kwenye mechi dhidi ya Simba na ile ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika mchezo mwingine.
Kipa huyo amesema ana uwezo wa kuokoa penati sita kati ya kumi anazopigiwa, na hivi karibuni ameokoa mbili, ikiwemo moja kwenye mechi kati ya Namungo na Azam FC.
“Mchezo dhidi ya Simba walipata penati tatu, nilifanikiwa kudaka ile ya Ateba, lakini penati ya Jean Charles Ahoua ilikuwa ngumu sana. Ni mchezaji ambaye amenipa wakati mgumu zaidi kwenye ligi, maana amepiga penati mbili dhidi yangu na zote nimeshindwa kuzizuia,” alisema Nahimana.
Ameeleza kuwa anaendelea kujifua zaidi kwenye kudaka penati, akiamini kuwa mafanikio aliyopata katika michezo hiyo miwili yamemjenga kisaikolojia na kuongeza kujiamini kwake langoni.
Kutokana na uwezo wake mzuri, Nahimana alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi katika mchezo dhidi ya Azam FC uliochezwa Alhamisi, Februari 27, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.