
KOCHA Mpya wa Taifa Stars Hanour Janza, ameomba sapoti ya Watanzania ili kuifikisha mbali timu hiyo katika harakati za kufuzu mashindano mbalimbali inayoshiriki.
Akizungumza na Spotileo, kocha huyo raia wa Zambia ameeleza furaha yake kupata nafasi hiyo lakini pia amewataka wachezaji Watanzania kuonesha bidii kulipigania taifa lao.
“Naishukuru TFF kwa kuona mimi ndio mtu sahihi kufundisha timu yao, naahidi kutumia ujuzi wangu wote ili tuweze kufikia malengo kitu cha msingi ni sapoti kutoka kwa viongozi na Watanzania wenyewe ambao ndio mashabiki wetu,” amesema Janza.
Kocha huyo amesema Taifa Stars siyo timu mbaya kwani Tanzania imebarikiwa vipaji vingi vya wacheza soka kazi kubwa iliyopo ni kuwaongezea vitu vidogo ambavyo vitawawezesha kucheza kwa malengo na kupata wanachokitaka.
Mtihani wa kwanza kwa Janza utakuwa Septemba 3 wakati Taifa Stars itakapokuwa ugenini Uganda kurudiana na wenyeji wao ‘The Cranes’ katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za michuano inayowashirikisha wachezaji wanaocheza soka kwenye ligi za ndani(CHAN).
Agosti 29 TFF ilifikia makubaliano ya kumuondoa aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen kwenye benchi la ufundi pamoja na wasaidizi wake.