Italia yawekewa ‘vingingi’ WC 2026

ZURICH: TIMU ya taifa ya Italia itaanzia nyumbani dhidi ya Ireland ya Kaskazini katika michezo ya mchujo ya kufuzu Kombe la Dunia mwezi Machi mwakani, lakini safari yao ya kurejea kwenye fainali hizo baada ya kukosa mara mbili mfululizo inaweza kuhitaji ushindi ugenini.
Hii ni baada ya FIFA kuchezesha droo ya michezo ya mechi hizo leo Alhamisi, ambapo mshindi kati ya Italia bingwa mara nne wa dunia na Ireland ya Kaskazini tarehe 26 Machi atalazimika kusafiri kucheza na mshindi kati ya Wales na Bosnia-Herzegovina siku tano baadae.
Italia haijacheza Kombe la Dunia tangu 2014 na ililazimishwa kwenda kwenye mechi za Playoff baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi lililotawaliwa na Norway.

Katika mechi nyingine za Playoff za Ulaya, Ukraine wataikaribisha Sweden, na mshindi atakuwa mwenyeji wa Poland au Albania kwenye mchezo wa fainali.
Njia ya Kosovo kufikia Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa ikiwa bado taifa changa zaidi barani Ulaya kisoka inaanza kwa mchezo wa ugenini dhidi ya Slovakia, kabla ya kuwa wenyeji wa mshindi kati ya Uturuki na Romania.
Ireland, ambayo imeandika historia kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Ureno na Hungary katika michezo miwili mfululizo wiki iliyopita, imepangwa kucheza nusu fainali ya Playoff dhidi ya Czech Republic ugenini. Mshindi wa mchezo huo atakuwa mwenyeji wa Denmark au North Macedonia katika hatua ya mwisho.
FIFA pia imefanya droo ya Playoff ya mabara sita kwa mataifa yasiyo ya Ulaya, ambapo washindi wake watafuzu kupitia njia ya intercontinental playoffs.




