Isak, Newcastle hapatoshi

MANCHESTER: Mshambuliaji wa Newcastle United Alexander Isak ameituhumu klabu hiyo kwa kuvunja ahadi na kuwahadaa mashabiki katika taarifa yake aliyoichapisha kwenye ‘story’ ya mtandao wa kijamii wa Instagram usiku Jumanne taarifa iliyothibitisha kuwa anataka kuondoka katika klabu hiyo.
Taarifa za ndani zinasema kuwa Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliutaarifu uongozi wa Newcastle kuhusu nia yake ya kuondoka klabuni hapo muda mrefu uliopita na kuahidiwa ushirikiano lakini hali imekuwa tofauti.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden ambaye alitengewa dau la pauni milioni 110 na Liverpool mapema mwezi huu ametajwa katika kikosi bora cha Ligi Kuu cha PFA msimu wa 2024/25. Hata hivyo, alichagua kutohudhuria sherehe hiyo kutokana na masuala yanayoendelea kuhusu mustakabali wake.
“Ahadi zinapovunjwa na uaminifu kupotea, uhusiano hauwezi kuendelea. Mabadiliko ni kwa maslahi ya kila mtu, sio mimi tu.” – Isak aliandika.
“Nimekaa kimya kwa muda mrefu wakati wengine wakizungumza. Ukimya huu umeruhusu watu kusambaza taarifa za upande mmoja ingawa wanajua haziakisi kile kilichosemwa na kukubaliwa kwa siri,”.
“Ukweli ni kwamba ahadi zilitolewa na klabu ilijua msimamo wangu kwa muda mrefu. Kufanya kana kwamba masuala haya yameibuka juzi tu ni kupotosha.” – Aliendelea
Newcastle kwa upande wao wamejibu tuhuma hizo na kusema katika taarifa kwa umma kwamba hakuna ahadi yoyote iliyotolewa na afisa wa klabu kwamba Isak anaweza kuondoka katika dirisha hili la usajili.
“Jibu letu ni wazi kwamba Alex bado yuko chini ya mkataba na sisi. Tunataka kuwabakiza wachezaji wetu bora, lakini pia tunaelewa wachezaji wana matakwa yao na tunasikiliza maoni yao.”
“Kama alivyoelezwa Alex na wawakilishi wake, ni lazima muda wote tuzingatie maslahi ya Newcastle United, timu na mashabiki wetu katika maamuzi yote na tumekuwa wazi kuwa masharti ya mauzo hayajatimizwa msimu huu na hatuoni kama masharti hayo yatatimizwa hivi karibuni.”
“Hii ni klabu ya soka yenye mila za kujivunia na tunajitahidi kuendeleza hisia za furaha kwa familia ya Newcastle. Alex anasalia kuwa sehemu ya familia yetu na atakaribishwa tena atakapokuwa tayari kuungana na wachezaji wenzake kikosini.” – Newcastle imesema.
Isak alikosa mechi ya kwanza ya Ligi kuu kati ya Newcastle dhidi ya Aston Villa katika mchezo ambao timu hizo hazikufungana mapema Jumamosi, na vijana hao wa Eddie Howe wanatarajiwa kucheza na mabingwa watetezi Liverpool Jumatatu.