Irene Uwoya: Mafanikio hupatikana ni maombi na matendo

DAR ES SALAAM: MREMBO kutoka kiwanda cha filamu nchini, Irene Uwoya, maarufu kama Mama Mchungaji, ametoa wito kwa Watanzania kuunganisha maombi na matendo ili kufanikisha maisha yenye baraka.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Uwoya ameandika amesikia kutaka kuzungumza na Watanzania kuhusu namna ya kufanikisha ndoto zao.
“Najua wengi tunatamani maisha mazuri, afya njema, ndoa za baraka, lakini nataka kuwaambia: kila kitu unachoomba hakikisha unakiishi,” ameandika.
Uwoya alisisitiza kuwa haiwezekani mtu akaomba afya njema lakini akawa anaishi maisha ya uharibifu.
“Haiwezekani wewe ukakesha club, pombe na mashisha, bangi sijui sigara halafu unamuomba Mungu afya njema… nakwambia utakufa,” amesema.
Kadhalika aliwataka vijana na wanawake kuacha kuamini kuwa mafanikio yatakuja kwa miujiza bila juhudi binafsi.
“Huwezi kutaka maisha mazuri lakini hufanyi kazi, hujiongezi kutafuta. Ukisubiri miujiza pekee, utakufa maskini ombaomba. Piga goti, lakini pia jitume,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa wale wanaotegemea wanaume kama njia ya kufanikisha maisha yao, wabadili fikra hizo.
“Amka kwenye hiyo ndoto, haitakaa itokee. Mungu akabariki kazi za mikono yetu, sasa hufanyi kazi hizo baraka utazitoa wapi?” amehoji.
Uwoya pia amewakumbusha wanaoomba ndoa njema kuzingatia mienendo yao.
“Ukiomba mume bora lakini unakesha club, unatukana watu, unadharau watu, na hujishughulishi na maisha, basi maombi yako hayatafanya kazi,” ameandika.
Mwisho, amewataka Watanzania kuhakikisha matendo yao yanaendana na maombi yao.
“Mungu hufanya hakika, ila kwa wenye juhudi ya maombi na kazi pia. Hakuna muujiza bila hatua. Nimeandika kwa upendo na kama nimekwaza naomba msamaha. Roho Mtakatifu alinisukuma niseme leo,” amesema.
Katika ujumbe wake, Uwoya amenukuu maandiko ya Biblia ikiwemo Mithali 20:13, Wakorintho 6:19-20, na Kumbukumbu la Torati 28:1-19, akisisitiza kuwa baraka za Mungu zinahusiana na matendo na bidii ya kila mtu.
Ujumbe wake umeibua hisia tofauti mitandaoni, lakini msisitizo wake unabaki wazi: Mafanikio ya kweli hupatikana kwa mchanganyiko wa maombi, imani na juhudi binafsi.