Nyumbani

Ilemela na uwekezaji mkubwa wa soka kwa vijana

YALE mawazo kwamba Tanzania itaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu katika
maendeleo ya soka huenda yakaanza kutoweka katika Mkoa wa Mwanza.

Hii ni baada ya kuwepo kwa uwekezaji mkubwa wa mamilioni katika soka kwa vijana katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ambao umetokana na juhudi kubwa za Mfuko wa Wakfu wa Angeline, yaani Angeline Foundation, Mbunge wa Jimbo la Ilemela na wadau wa
maendeleo ya soka.

Hii ni habari njema si tu kwa wadau wa soka katika Manispaa ya Ilemela -Mwanza, bali pia kwa taifa kwa ujumla kwa sababu kuwepo kwa ligi hiyo kumeleta mafanikio makubwa ya soka kwa vijana na taifa.

Hii inatokana na baadhi ya wanamichezo kujiajiri wao wenyewe na baadhi yao kuchukuliwa na timu kubwa na mahiri duniani na pia Angeline Mabula Jimbo Cup inaendelea kuwajenga vijana kimaadili na kiuzalendo.

Hii ni kwa sababu katika dunia ya sasa, licha ya michezo kuwa ni afya inakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, taasisi na wa taifa kupitia mapato yatokanayo na michezo.

Imekuwa ni ya manufaa kwa sababu hivi sasa uwekezaji katika soka una gharama kubwa katika kuibua vipaji vya vijana vinavyochipukia, ambavyo vinakabiliwa na changamoto lukuki, zikiwemo za uhaba wa viwanja na wafadhili na utayari wa wadau wengine katika kuwekeza katika soka na michezo mingine.

HISTORIA YA UWEKEZAJI
Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Angeline Mabula anasema wazo la uwekezaji wa soka kwa vijana katika jimbo lake lilianza miaka saba iliyopita.

Anasema lengo la uwekezaji huo likiwa ni kuwaleta vijana pamoja, kufahamiana ili kujadili mambo ya msingi kwa ajili ya ustawi wa maisha yao kupitia michezo, kuwajenga kimaadili, kuwawezesha kupata ajira, kujenga umoja na mshikamano kupitia soka na kupata fursa ya kujadili mambo muhimu kwa ajili ya ustawi wa maisha yao kupitia mchezo huo.

“Nafurahi sasa ni takribani miaka saba, kwa mchango wangu na wa wadau wa soka mkoani Mwanza kwa pamoja tumefanikiwa kuanzisha mashindano ya soka maarufu kama Angeline Mabula Jimbo Cup,” anasema na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia
na kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha michezo nchini.

Anasema Angeline Jimbo Cup (AJC) kwa kushirikiana na Angeline Foundation imekuwa ikiandaa mashindano ya aina mbalimbali tofauti na soka mfululizo kila mwaka tofauti
na mwaka ambao taifa lilikumbwa na ugonjwa wa Covid-19 ikiwa pia ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ibara ya 242 na ukurasa wa 291-292 inayosisitiza umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya na uchumi.

Anasema uwekezaji huo ambao hugharimu kiasi cha takribani Sh milioni 35 kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu ya kidijitali zaidi, hufanyika katika ngazi ya kata kwa kuhusisha mitaa yote ambapo kwa ngazi ya jimbo yanahusisha jumla ya timu 20 kutoka kata zote 19 za Jimbo la Ilemela.

Anasema timu 20 kwa kata hizo zinahusisha mpira wa miguu kwa wavulana, timu nane mpira wa miguu kwa wasichana, timu saba za volleyball ikiwa na wanaume watano na wanawake wawili, mpira wa pete timu zinazoshiriki ni nane, timu 19 za karata na timu 19 za drafti zikiwa ni kutoka kata zote katika Jimbo la Ilemela.

MAFANIKIO YA SOKA (AJC)
Mabula anasema kuanzishwa kwa AJC kumeleta mafanikio makubwa hususani katika soka la vijana, hali iliyowafanya vijana kujiamini, kujitathmini na kujitambua. Anayataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuibuliwa kwa vipaji bora vya vijana katika soka, ambao
kwa sasa wanacheza katika klabu mbalimbali nje ya nchi.

Anawataja vijana hao wanaocheza katika klabu za nje kuwa ni Kelvin John anayechezea
timu ya Genk iliyoko Ubelgiji, Andrew Michael ambaye kwa sasa anachezea timu ya Al Rams Khamia -Dubai, Jackson Simba anachezea timu ya San Diego–California -Marekani na James Dams James yuko timu ya Genk nchini Ubelgiji.

Anasema hata hivyo AJC imefanikiwa pia kuibua vipaji vya wachezaji wengine wapya
ambao wanatarajiwa kuondoka hivi karibuni kwenda nchi mbalimbali kwa ajili ya mechi za
majaribio.

Anawataja wachezaji hao kuwa ni Machumu Shuba, Edward Joseph, Rajab Joseph,
Michael Aloyce na Jackson Peter ambaye aliibuliwa katika msimu wa sita wa Angeline Jimbo Cup 2023 kwenye hatua ya makundi ambao wote kwa sasa wamekwenda nchini Mali katika Kituo cha kuendeleza vipaji cha Sports Republic kinachosimamia timu ya Southamption ya Uingereza.

“Wanatarajia kuondoka muda wowote wanachosubiri ni viza,” anasema. Anasema mchezaji Jackson anakwenda kujiunga na timu ya Dar City inayoshiriki Ligi Daraja la Pili na kuyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa michezo miwili ya soka na mpira wa pete na kufikia michezo saba na kuongeza hamasa na mvuto zaidi kwa jamii kupitia Angeline Jimbo Cup.

Anasema mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuwa Ilemela Jimbo Cup imesaidia kuwaleta wana Ilemela pamoja kutoka maeneo mbalimbali na kutoa fursa ya kubadilishana mawazo.
Kwa upande wa changamoto anasema AJC inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ya mwitikio mdogo wa kutoka baadhi ya maeneo, ingawa changamoto hizo zimekuwa zikitumiwa kama fursa ya kujijenga zaidi.

MCHEZAJI ANENA
Mchezaji wa zamani wa Simba, Andrew Michael akiwa ni mmoja wa wanamichezo
walioibuliwa na AJC, ambaye kwa sasa anasakata kabumbu katika Klabu ya Al Rams
Khamia -Dubai, anasema amepata mafanikio makubwa ya kisoka kupitia AJC.

“Mashindano ya Angeline Mabula Jimbo Cup ni mazuri ndiyo yaliyonifikisha hapa nilipo leo, namshukuru Mama Mabula kwa moyo wake wa upendo na uthubutu wa kufanya mambo,” anasema.

Anasema AJC imewaibua vijana mbalimbali wenye vipaji kama Mashi Kigiri aliye Singida United, Hassan Kibairo –Coastal Union na kudai kuwa na yeye ni miongoni mwa watu waliopata mafanikio makubwa.

Michael anasema Mabula pia amekuwa ni msaada mkubwa kwenye kituo chao cha Football House tangu kuanzishwa kwake hadi sasa ambaye amekuwa akiwapatia huduma za chakula na vifaa muhimu vya michezo.

“Tunamshukuru Mama na pia tunamuunga mkono katika mashindano haya ambayo nikiri yametusaidia kukamilisha ndoto zetu za kufika mbali  kisoka,” anasema.

Related Articles

Back to top button