Haller mguu nje, mguu ndani AFCON 2025

RABAT: MSHAMBULIAJI Sebastien Haller, aliyefunga bao muhimu lililoipa Ivory Coast taji la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) lililopita, yupo hatarini kukosa michuano ya mwaka huu nchini Morocco kutokana na majeraha.
Haller alipata jeraha la msuli wa paja (hamstring) alipokuwa akiichezea klabu ya Utrecht katika ligi ya Uholanzi mwishoni mwa wiki, na tangu ajiunge na kambi ya maandalizi ya timu ya taifa ya Ivory Coast mjini Marbella, Hispania, amekuwa akifanyiwa matibabu.
Shirikisho la soka la Ivory Coast limesema bado linasubiri majibu ya vipimo vya kitabibu kabla ya kufanya uamuzi kuhusu upatikanaji wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31.
Haller pia alikosa mechi za mwanzo za AFCON 2023 kutokana na jeraha la kifundo cha mguu, lakini alirejea katika hatua za mtoano na kufunga bao la ushindi kwenye nusu fainali na fainali, akiiwezesha Ivory Coast kutwaa ubingwa.
Ivory Coast itaanza kutetea taji lake kwa kucheza dhidi ya Msumbiji mjini Marrakech Jumatano ijayo.




