Kwingineko

Gwajima: Wanawake wapewe nafasi michezo na biashara

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, ametoa wito wa kuendelea kumpa nafasi mwanamke kushiriki kikamilifu kwenye majukwaa ya michezo na biashara akisisitiza mchango wake katika uchumi na maendeleo ya familia.

Akizungumza katika mbio za riadha za kuadhimisha miaka 20 ya Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) Dar es Salaam, Dk Gwajima amesema ni wakati wa jamii kutambua uwezo mkubwa wa wanawake, si tu katika biashara bali pia katika michezo.

“Tumeona wanawake wanavyoweza kushiriki kwenye mbio za riadha. Kukimbia kilomita 21 ni sanaa, ni afya na ni mazoezi. Huu ni uthibitisho kuwa mwanamke anaweza,” amesema Dk Gwajima.

Amesema kuwa mwanamke ni mhimili wa uchumi wa familia na taifa kwa ujumla, hivyo anastahili kupewa fursa sawa katika majukwaa ya biashara kama ilivyo kwa TWCC, taasisi inayowaunganisha na kuwawezesha wanawake wafanyabiashara nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Dar es Salaam (DAA), Aman Ngoka, amesema mbio hizo zimefungua milango kwa vijana kutoka mikoa mbalimbali kuonesha vipaji vyao.

Ngoka amesema mashindano ya aina hiyo yanasaidia kuibua vipaji vipya na kurahisisha mchakato wa kuvifuatilia na kuviendeleza kwa manufaa ya taifa.

“Hatuwezi kufanya kazi peke yetu. Tunapaswa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazotaka kuandaa mbio za riadha hapa Dar es Salaam kwa sababu tunatambua umuhimu wake katika kuibua wanariadha wapya,” amesema.

Maadhimisho ya miaka 20 ya TWCC yamekuwa si tu jukwaa la kusherehekea mafanikio ya wanawake katika biashara, bali pia kuhamasisha afya, mshikamano na ushiriki wa wanawake katika michezo, hususan riadha.

Related Articles

Back to top button