Gumzo la Fei Toto, Azam FC watoa kauli

DAR ES SALAAM: KATIKA kipindi hiki cha mvutano wa usajili na tetesi mbalimbali, jina la kiungo mahiri wa Azam FC, Feisal Salum, `Fei Toto`, limeendelea kuibua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka nchini.Hii ni kufuatia kutajwa kwake kuwindwa na klabu kongwe za hapa Tanzania, Yanga na Simba.
Meneja wa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit ‘Zaka za Kazi’, amevunja ukimya na kuweka wazi msimamo wa klabu hiyo juu ya hali ya mchezaji huyo amesema hadi sasa hakuna klabu yoyote iliyowasilisha ofa rasmi kwa ajili ya kumsajili Fei Toto, wala mchezaji mwingine kutoka kikosi chao.
“Fei Toto ni miongoni mwa wachezaji wetu muhimu na hatumuweka sokoni na kama klabu hatujapokea ofa yoyote rasmi kutoka timu yoyote iwe ni ndani au nje ya nchi,” amesema Zaka.
Tetesi zimekuwa zikimhusisha Fei Toto kurejea Yanga, klabu aliyoitumikia kabla ya kujiunga na Azam, hasa baada ya taarifa za kuondoka kwa kiungo wao tegemeo, Stephane Aziz Ki. Vilevile, Simba wametajwa kuwa na nia ya kumvuta nyota huyo kwa maandalizi ya msimu ujao.
“Sisi hatumzuia mchezaji kuondoka endapo kutakuwa na ofa nzuri inayokidhi makubaliano ya kimkataba. Hata alipondoka Prince Dube, tuliheshimu makubaliano. Hivyo msimamo wetu uko wazi,” ameongeza.




