Guardiola asifu usajili mpya City

PHILADELPHIA: Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesifu kiwango kilichooneshwa na wachezaji wapya waliosajiliwa na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi kilichoilaza 2-0 Wydad Casablanca katika mechi yao ya ufunguzi kwenye Kombe la Dunia la Klabu linaloendelea nchini Marekani.
Kiungo wa kati wa Uholanzi Tijjani Reijnders na kiungo mshambuliaji wa Ufaransa Rayan Cherki walianza katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Lincoln Financial Field mjini Philadelphia baada ya kujiunga na Man City kutoka AC Milan na Lyon.
“Yeye (Reijnders) ni mchezaji mzuri sana. Unaweza kuhisi hilo. Kasi yake katika eneo la mpinzani akiwa na mpira inaridhisha atakapopata moto zaidi, hatakuwa mchezaji wa kawaida,” – alisema Guardiola
Akiletwa kusaidia kuziba pengo kubwa lililoachwa na Kevin De Bruyne, Rayan Cherki mwenye miaka 21 alikichafua kwa takriban dakika 60 kabla ya kufanyiwa mabadiliko wakati City walipohitaji kupunguza kasi baada ya kupata ushindi kutokana na mabao ya kipindi cha kwanza ya Phil Foden na Jeremy Doku.
“Kwa kweli ni ngumu kupata mtu wa kuvaa viatu vya Kevin tunajua hilo kutokana na ubora alionao hakuna shaka juu ya hilo lakini klabu iliamua kumleta Rayan kwa sababu ana ujuzi wa ajabu akiwa kwenye box ana maono na anaweza mambo mengi. Huu ulikuwa mchezo wake wa kwanza tu, katika hali ngumu sana, na nimefurahishwa sana kuwa tunaye hapa.” Guardiola aliongeza.
Kulikuwa na sura ya majaribio kwa kikosi cha City dhidi Wydad huku beki chipukizi wa Brazil Vitor Reis akianza kwa mara ya tatu tangu asajiliwe Januari huku Nathan Ake akiichezea klabu yake kwa mara ya kwanza tangu mwishoni mwa Februari.