Grealish: Mlitaka nifanye nini?

MANCHESTER: WINGA wa Manchester City, Jack Grealish amewajibu wakosoaji kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mustakabali wake ndani ya kikosi cha Manchester City baada ya tetesi kuwa nyota huyo ataachwa katika kikosi kitakachosafiri kwenda Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia la Klabu baadae mwezi huu.
Kituo cha Televisheni cha Sky Sports News nchini England kiliripoti kuwa Grealish anatarajiwa kutojumuishwa kwenye kikosi cha Pep Guardiola kitakachoshiriki Kombe la Dunia la Klabu taarifa iliyozua maoni mseto miongoni mwa wadau wa soka nchini humo.
Nahodha huyo wa zamani wa Aston Villa, ambaye aliigharimu Manchester City pauni milioni 100 mwaka 2021, pia hakuwa sehemu ya kikosi cha Pep kilichoivuruga Fulham mabao 2-0 katika siku ya mwisho ya msimu wa ligi kuu ya England.
Ni uamuzi huu ambao ulipelekea Gabriel Agbonlahor, mchezaji mwenza wa zamani wa Grealish kutoka Villa kwenye mahojiano na TalkSport, kumshutumu kocha Pep Guardiola kwa kuchukulia suala hilo kama suala binafsi licha ya bosi huyo wa City kusisitiza kwamba lilikuwa ni suala la kawaida la uchaguzi wa kikosi kuelekea kwenye kila mechi.
Akijibu chapisho la TalkSport lililomnukuu Agbonlahor akizungumzia jinsi Pep anavyomnyanyasa mchezaji wake huyo. Grealish alikuja kwenye uwanja wa ‘comment’ kwenye post hiyo na kujibu “Ulitaka nifanyeje? Nifunge ‘hatty’(hat-trick) ndani ya dakika20?”.
Hakuishia hapo Grealish aliijibu moja ya comment ya shabiki aliyesema winga huyo amekuwa na kiwango kibovu siku za karibuni akisema “Haha, nimekuwa na kiwango duni? Nimefunga mabao matatu kwenye mechi tatu nilizocheza zaidi ya dakika 45 lakini ni sawa…”
Licha ya kubakiza miaka miwili kwenye mkataba wake na Manchester city Grealish amekuwa akihusishwa na kuhamia klabu nyingine za Ligi Kuu ya England na nje ya nchi hiyo baada ya kuanza michezo saba pekee kwenye ligi kuu msimu uliomalizika.