Nyumbani

Geita Gold: Msimu Haujaisha, Vita ya Mtoano Inaanza

DAR ES SALAAM: KLABU ya Championship ya Geita Gold imesema msimu kwao bado haujaisha wanaelekeza nguvu katika mchezo wa mtoano dhidi ya Stand United kutafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu.

Timu zilizomaliza nafasi ya tatu na nne kwenye Ligi ya Championship zinacheza hatua ya mtoano zenyewe kisha mshindi atakutana na timu ya Ligi Kuu zitakazoingia katika mtoano.

Geita ilimaliza nafasi ya nne itacheza na Stand United iliyoko katika nafasi ya tatu katika mchezo wa kwanza utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kisha wa marudiano utachezwa ugenini Shinyanga.

Kwa mujibu wa msemaji wa klabu, Samwel Didas, Geita bado ina kazi moja kubwa mbele, wanataka kumaliza kazi nyumbani kuhakikisha wanafanya vizuri kwa ushindi mkubwa kabla ya kwenda ugenini.

“Lazima nikubali, haikuwa dhamira ya msingi kwa timu hii kufika mtoano. Tulipanga moja kwa moja kurudi Ligi Kuu, lakini hali imekuwa tofauti. Hatuwezi kukata tamaa badala yake, tunapambana kwa nguvu mpya kwa sababu bado tuna nafasi ya kurudi Ligi Kuu kupitia mtoano,

“Tunataka kuimaliza kazi hii hapa nyumbani. Tumejipanga kuhakikisha tunashinda mchezo wa kwanza kwa kishindo,” alisisitiza msemaji huyo.

Didas anasema kikosi kipo imara na kina uwezo wa kupambana na timu yoyote hata zile kutoka Ligi Kuu.

Katika hatua ya kuwahamasisha mashabiki, uongozi wa Geita Gold umechukua hatua ya kipekee kwa kununua tiketi za mashabiki ili kuwawezesha mashabiki kuingia bure.

Related Articles

Back to top button