Mtihani wa kwanza wa Gamondi huu hapa

DAR ES SALAAM: BAADA ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumtangaza Miguel Gamondi kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, ataanza kibarua chake cha kwanza katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Kuwait.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Novemba 14, mwaka huu katika Uwanja wa Al Salam, jijini Cairo nchini Misri ikiwa ni kipindi cha Kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA).
Gamondi ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, alitangazwa jana kukaimu nafasi iliyoachwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyesitishiwa mkataba.
Katika viwango vya FIFA, Tanzania inashika nafasi ya 107, wakati Kuwait ni ya 135.
Kocha huyo ikiwa ni siku moja imepita tangu atangazwe kushika nafasi hiyo aliandika ujumbe huu kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii:
“Safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja. Zingatia hatua iliyo mbele yako, si ngazi nzima. Chukua hatua ndogo kila siku, kwani kila siku ni nafasi mpya ya kuwa bora zaidi. Kumbuka, wewe ndiye mpaka wako pekee.”
Mwisho




