Nyumbani

Gamondi amrejesha Kelvin John Stars

DAR ES SALAAM: KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi, ametangaza kikosi cha wachezaji 23 watakaoingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa kalenda ya FIFA dhidi ya Kuwait, utakaochezwa Novemba 14, 2025 jijini Cairo, Misri.

Kati ya mambo yaliyovutia zaidi katika orodha hiyo ni urejeo wa mshambuliaji Kelvin John, anayekipiga katika klabu ya Aalborg BK ya Denmark, ambaye anarejea Stars baada ya takribani miezi nane nje ya kikosi hicho.

Kelvin aliitwa kwa mara ya mwisho mwezi Machi mwaka huu, chini ya aliyekuwa kocha wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, wakati timu hiyo ikijiandaa na mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco.

Uamuzi wa Gamondi kumrejesha mchezaji huyo umeonekana kuwa wa kimkakati, ukizingatia kiwango bora alichoonesha akiwa Aalborg BK, ambapo mpaka sasa ametupia mabao saba na kutoa pasi tatu za mabao kwenye mechi 15 za Ligi Daraja la Kwanza Denmark msimu wa 2025/26.

Gamondi amesema wachezaji wataanza kambi rasmi Novemba 10, ambapo watajipima dhidi ya Kuwait kama sehemu ya maandalizi ya michezo ya kufuzu Kombe la Dunia na michuano mingine ya kimataifa.
Kikosi hicho pia kimejumuisha nyota mbalimbali wanaocheza ndani na nje ya nchi, akiwemo Yakoub Suleiman (Simba), Bakari Mwamnyeto (Yanga), Novatus Dismas (Goztepe – Uturuki), Haji Mnoga (Salford City – Uingereza), Tarryn Allarakhia (Rochdale – Uingereza) na Charles M’mombwa (Floriana – Malta).

Wengine ni Zuberi Foba (Azam FC), Hussein Masalanga (Singida Black Stars), Feisal Salum (Azam FC), Mudathir Yahya (Yanga), Suleiman Mwalimu (Simba), Paul Peter (JKT Tanzania), na Morice Abraham (Simba).

Related Articles

Back to top button