EPL

Gabriel aota makombe akiongeza miwili Arsenal

LONDON: Beki wa kati wa Arsenal, Gabriel Magalhaes amesaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia katika viunga vya Emirates hadi 2029. Mbrazil huyo tayari alikuwa anatumikia mkataba ambao ulikuwa unatamatika 2027 na kitendo cha beki huyo kuongezewa mkataba kinaashiria umuhimu wake kwenye ‘project’ ya meneja Mikel Arteta.

Gabriel amekuwa mchezaji muhimu wa Arsenal tangu ajiunge na klabu hiyo kwa uhamisho wa Euro milioni 27 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 75.6 kutoka Lille ya Ufaransa mwaka 2020, akicheza mechi 210 katika mashindano yote.

“Nilifika hapa nikiwa mchezaji mdogo na baada ya takriban miaka mitano nina furaha sana na nimejifunza mengi. Imekuwa safari nzuri, na kwakweli ninafurahi kuiendeleza. Natumai nitashinda mataji kadhaa na klabu hii, kwa sababu naipenda na familia yangu inaipenda pia” – alisema Gabriel.

“Arsenal ni klabu ya nzuri na ninajivunia kusaini mkataba mpya. Ninawapenda mashabiki wote, wachezaji wenzangu, naupenda uwanja huu. Asante kwa sapoti yote mlionipa na sasa tueendelee pamoja.” aliongeza

Tangu 2022 Gabriel amekuwa na muunganiko mzuri sana na beki mwenzie William Saliba katika safu ya katikati ya ulinzi, huku wakidhihirika kuwa tishio kwa washambuliaji wanaokutana nao lakini pia kwa mipira ya kutenga.

Gabriel alikosa miezi miwili ya mwisho ya msimu uliomalizika wa 2024/25 kutokana na jeraha la msuli wa paja na ikaonekana wazi kukosekana kwake kuliiondoa Arsenal katika mbio za kuwania taji la Premier League na kushindwa katika nusu-fainali ya UEFA Champions League na baada ya kutupwa nje na mabingwa wapya Paris St-Germain (PSG).

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button