Europa

Forest na historia yatinga robo fainali Europa League

LONDON, England: NOTTINGHAM Forest imeandika historia mpya barani Ulaya baada ya kutinga robo fainali ya Europa League kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996, licha ya kupitia msimu mgumu katika Ligi Kuu England.

Forest ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 3-0 dhidi ya Midtjylland ya Denmark, kufuatia jumla ya mabao 2-2 katika michezo miwili.

Ushindi huo mkubwa umekuja wakati ambao Forest imekuwa ikikumbana na changamoto nyingi msimu huu, ikiwa inapambana kujinasua kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja na ikibadilisha makocha mara kwa mara hadi kufikia kocha wa nne, Vitor Pereira.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa MCH Arena, Herning, Denmark, mashabiki wa Forest waliokuwa wamejazana ugenini walipata sababu ya kushangilia baada ya timu yao kupindua matokeo ya kufungwa 1-0 katika mechi ya kwanza.

Ushindi huo pia umefuta kumbukumbu ya miezi mitano iliyopita, ambapo mashabiki wa Forest waliizomea timu yao baada ya kufungwa mabao 3-2 nyumbani dhidi ya wapinzani hao hao chini ya kocha Ange Postecoglou.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button