Fadlu: Tumekosa wachezaji kama wa Yanga

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amefunguka baada ya timu yake kupoteza mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, kwa mabao 2-0 kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Jumatano Juni 25.
Kocha huyo amesema kikosi chake kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wachezaji wenye ari ya kupambana, hasa kwenye mechi kubwa kama hiyo.
Fadlu hakusita kuipongeza Yanga kwa ushindi na kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo.
Amesema mafanikio hayo si ya bahati bali ni matokeo ya kikosi bora kilichojaa wachezaji wenye morali ya hali ya juu na uwezo wa kucheza mechi zenye presha kubwa.
“Tunahitaji kuboresha kikosi chetu. Yanga wameonesha ubora mkubwa, wamekuwa na wachezaji wanaojitoa kwa moyo na wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za mechi kama hizi. Hicho ndicho tunachokikosa sisi,” amesema.
Fadlu amekiri kuwa matokeo hayo hayakuwa sehemu ya matarajio yao lakini amesisitiza kuwa, kwa hali ya kikosi walichonacho, wamevuka malengo kwa kiwango fulani msimu huu.
Amesema bado ana imani na mchakato wa kujenga timu imara kwa msimu ujao.
“Tulitegemea ushindani mkubwa na kwa bahati mbaya hatukuweza kufikia kiwango hicho. Hata hivyo, kikosi tulichokuwa nacho tumefanikwa kuvuka baadhi ya malengo yetu. Tunahitaji kurekebisha mapungufu haya kuelekea msimu mpya,” ameongeza.
Hii ni mara ya tano mfululizo kwa Simba kupoteza dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa watani wa jadi, jambo ambalo linaweka presha kwa benchi la ufundi la Simba kuja na suluhisho la kudumu.
Fadlu amesisitiza kuwa maboresho makubwa yanahitajika ili kurejesha Simba kwenye ushindani wa hali ya juu msimu ujao.