Fadlu aisoma ramani ya Yanga

DAR ES SALAAM: LICHA ya Yanga kudai kuwa hawatashiriki Kariakoo Derby itakayopigwa Jumapili, Juni 15, Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, ameibuka na kusema wazi kuwa amewashtukia watani wao na ana uhakika kuwa nao wanajiandaa kimyakimya kwa mchezo huo wa kukata na shoka.
Fadlu, raia wa Afrika Kusini, amesema Simba haipo usingizini, bali imeingia kwenye kambi maalum ya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya pambano hilo lenye mvuto mkubwa, akieleza kuwa mechi hiyo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuamua bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
“Tunajua wapinzani wetu wanajiandaa, hata kama hawasemi. Hii ni mechi kubwa. Tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi zote tatu. Ni hatua muhimu kuelekea kwenye ubingwa,” amesema.
Kocha huyo amesema baada ya Simba kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, nguvu zao zote sasa zimeelekezwa kwenye ligi ya ndani, ambapo matarajio ya kutwaa taji la Ligi Kuu yako juu.
“Wachezaji wangu wako fiti kimwili na kiakili. Tumefanya kazi kubwa kuboresha nidhamu ya kiufundi, kasi na mpangilio wa mashambulizi. Hili derby si la kawaida, ni zaidi ya mchezo ni vita ya heshima na historia,” ameongeza.
Amesisitiza kuwa Simba haitaruhusu presha iwatawale, bali wataingia uwanjani kwa utulivu, mbinu madhubuti na ari ya ushindi. Anasema wanataka kuonesha soka safi la kisasa, ambalo litathibitisha ukuu wa timu hiyo mbele ya watani wao.
“Hatutaki kushinda kwa sababu tu ya ushindani wa jadi. Tunahitaji pointi hizi kwa mustakabali wa ubingwa. Ni lazima tucheze kwa akili na uthubutu mkubwa,” amesema Davids.
Mbali na maandalizi ya ndani ya uwanja, Fadlu pia amewaalika mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi Jumapili hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, akiamini kuwa sapoti yao itakuwa nguzo muhimu kwa wachezaji wake kutimiza majukumu yao kikamilifu.
“Mashabiki ni sehemu ya nguvu zetu. Tunawahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Tuungane kuhakikisha Simba inapata kile inachostahili ushindi,” amesema.