BurudaniFilamu

EXTRACTION

AMEBARIKIWA kuwa na fedha nyingi sana lakini amenyimwa uhuru wa kuzitumia.

Ni tajiri haswa, ana watumishi wanaomtii na pia ana adui wengi. Ni muuza dawa za kulevya, Ovi Mahajan Sr aliyefungwa gerezani nchini India. Jela inamfanya atoe amri akiwa nyuma ya nondo.

Mahajan anaamrisha mtoto wake Ovi awekwe kwenye uangalizi wa hali ya juu mpaka yeye atakapotoka jela. Lakini haikuwa hivyo.

Kosa moja tu la kukosa umakini linamsafirisha mtoto Ovi mpaka Jiji la Dhaka nchini Bangladesh akiwa mikononi mwa adui mkubwa wa baba yake, Amir Asif, mtu katili sana, nusu mtu nusu shetani.

Hii ni baada ya muda wa shule, Ovi anatoroka kutoka nyumbani na kwenda klabu ambako anaishia kutekwa nyara na maofisa wa polisi wanaomfanyia kazi Amir Asif. Kama Mahajan anajiona bab kubwa nchini India, basi Asif ni mwasisi wa waasi wa Bangladesh.

Taarifa inamfikia Mahajan akiwa jela na anatoa amri, hata kwa gharama ya kitovu cha nchi anamhitaji mwanawe Ovi apatikane huku akitishia kuidhuru familia ya Saju Rav, opereta wa zamani wa Para (SF) na mlinzi wa Ovi.

Picha linaanzia hapo. Na ndipo anapoibuka mtu anayeitwa Tyler Rake, mamluki wa soko la magendo na opareta wa zamani wa SASR, mtu aliyepoteza kila kitu kwenye maisha yake na kubaki yeye na pumzi yake tu.

Rake anaandamwa na kumbukumbu za mtoto wake mwenyewe, ambaye alikufa akiwa na umri mdogo kutokana na tatizo la lymphoma na pia hajui mahali alipo mke wake, vyote vinamfanya aamue kuishi maisha yake, yasiyoogopa kufa.

Rake ni mafia wa kukodiwa, anaajiriwa na mamluki mwenzake Nik Khan, ili kumwokoa mtoto Ovi kutoka nchini Bangladesh… ni kazi inayohitaji kikosi kizima cha jeshi lakini anakwenda yeye. Bunduki zinamtii kila analosema na vita ndiyo maisha aliyochagua.

Rake anawekewa fedha mezani, anapewa wajibu wa kumrudisha mtoto Ovi kwa baba yake. Mwanamume huyo anaamua kuingia kazini. Anaamini fedha ndiyo kila kitu na anaamini kwenye uwezo wake wa mapambano.

Timu yake na Khan inajiandaa kumtoa mtoto Ovi na watu wa Mahajan, wakiongozwa na Saju wapo tayari kulipa mara tu Ovi atakapopatikana. Lakini siyo kazi rahisi, ni hapo Bangladesh ndipo Rake anaonja uchungu wa ugumu wa vita.

Anampata mtoto Ovi na anamwokoa baada ya kuwaua watekaji nyara wake, na kisha kumpeleka mahali pa siri, lakini anagundua kuwa amechezwa shere kwenye fedha na wanaotakiwa kumlipa.

Saju anawaua watu wa Rake ili amrudishe mtoto Ovi nchini India na kukwepa kulipa malipo yoyote kwa Rake. Inapogundulika kuwa mtoto Ovi ametoweka, Asif anaamuru kufungwa kwa mipaka ya Dhaka mara moja, na anaweka vizuizi kwenye madaraja yote nje ya jiji hilo.

Sasa Rake anabaki njia panda, hajui amuache mtoto Ovi na aondoke zake au awe na huruma japo fedha kaikosa. Mji wote umewekwa ‘lockdown’. Hakuna mahali anaweza kupita bila ya kujulikana.

Anahitajika akiwa hai na jeshi ndilo linachukua dhamana ya upatikanaji wake. Rake anahitaji kuwa ngangari kwelikweli mbele ya jeshi la waasi. Ni mtu mmoja dhidi ya nchi nzima. Anafunga mkanda na anamtaka mtoto Ovi amuamini.

Ovi anapojua kuwa yupo kwenye mikono salama anakuwa tayari kwa lolote huku akisikia milio ya risasi ikirindima masikioni kwake. Khan anaandaa helikopta ili kumtoa Rake nje ya jiji na kumwambia amtelekeze mtoto Ovi kwani hawatalipwa tena fedha hata wakimwokoa.

Rake anakataa, hasa anapokumbuka masaibu ya mtoto wake mwenyewe. Anapambana na genge la vijana linaloongozwa na Farhad, mhalifu kijana anayetaka kumfurahisha Asif.

Rake anampigia simu rafiki yake Gaspar, mstaafu mwenzake wa kikosi maalumu anayeishi Dhaka, kisha Rake na mtoto Ovi wanalala nyumbani kwa Gaspar. Gaspar anamtonya Rake kwamba Asif ameweka dau la dola milioni 10 kwa ajili ya mtoto Ovi, anataka wagawane ikiwa Rake atamruhusu kumuua Ovi.

Rake anakataa na kulianzisha kati yake na Gaspar, ambaye anapigwa risasi na Ovi. Rake yupo tayari kwa lolote, anaamua kuwa yeye afe lakini mtoto Ovi afike salama India. Anafanya yake wakati mtoto Ovi aliyejibadilisha sura anapitia katika kituo cha ukaguzi katika daraja, anahakikisha Ovi anavuka salama.

Wakati huo Khan na mamluki wake waliobaki wanasogea eneo hilo kutoka upande wa pili wa daraja tayari kuwapokea, muda huo Asif anachunguza eneo hilo kwa darubini kutokea mbali. Na hapa inapiganwa vita ya karne.

Rake anajeruhiwa, lakini anahakikisha Ovi yuko salama kwa kumtaka akimbilie kwenye helikopta ya Khan inayosubiri upande wa pili. Wakati Rake anamfuata, anapigwa risasi shingoni na Farhad, na wakati huo anaona kuwa Ovi yuko salama. Anaanguka ndani ya mto.

Mtoto Ovi, Khan na timu ya uokozi wanafanikiwa kukimbilia Mumbai. Miezi minane baadaye, Khan anamuua Asif kwenye choo cha wanaume. Ovi anarukia ndani ya bwawa la kuogelea la shuleni kwao na ndani ya maji anamwona mtu akimwangalia kwa makini. Hamwoni sawasawa lakini anafanana na Tyler Rake.

Kwa kweli Chris Hemsworth ameionesha dunia kwa nini yeye ni msanii wa pili kulipwa fedha nyingi duniani kwenye filamu. Hii ni moja kati ya filamu za aksheni zinazosisimua na zisizochosha kuzitazama… Imetoka rasmi mnamo Aprili 24, 2020 kwenye mtandao wa Netflix.

Baada ya kutoka filamu hii imepata maoni tofauti kutoka kwa wakosoaji, ambao wamesifia uchezaji na mfuatano wa matukio, lakini wamekosoa msuko wa hadithi na matukio mengi ya vurugu. Imekuwa ndiyo filamu inayotazamwa zaidi katika historia ya Netflix.

Related Articles

Back to top button