EPL
Enzo Maresca na Chelsea sasa basi!

LONDON:ENZO Maresca ameondoka rasmi Chelsea baada ya uongozi wa klabu na kocha huyo wa Italia kufikia makubaliano ya pande zote kuvunja ushirikiano wao, kufuatia matokeo mabaya na mvutano wa ndani uliodumu kwa muda. Maamuzi hayo yamethibitishwa na Chelsea siku ya Mwaka Mpya, wakisema mabadiliko hayo yamelenga kuipa timu nafasi bora ya kurekebisha msimu.
Maresca anakumbukwa zaidi kwa mafanikio yake ya awali Stamford Bridge, ikiwemo kuizuia PSG kutwaa rekodi ya mataji saba mwaka 2025, pamoja na kuiongoza Chelsea kushinda UEFA Conference League na Kombe la Dunia la Klabu. Pia aliisaidia timu kumaliza nafasi ya nne Premier League msimu uliopita na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika msimu huu baada ya Chelsea kushinda mechi moja tu kati ya saba za mwisho za ligi na kujikuta wakiwa pointi 15 nyuma ya vinara Arsenal.
Mbali na matokeo duni, kulikuwa na sintofahamu kati ya Maresca na viongozi wa klabu kuhusu masuala ya kurejesha wachezaji walioumia, pamoja na kauli zake za wazi kwamba baadhi ya watu ndani ya klabu hawakuwa wakimuunga mkono yeye na timu. Hali hiyo ilizidi kuibua maswali, hasa alipokosa kuhudhuria mkutano na waandishi wa habari baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Bournemouth, tukio lililotajwa kuwa ni ishara ya wazi ya matatizo ya ndani.
Ripoti pia zilichangia presha baada ya Maresca kuhusishwa na uwezekano wa kwenda Manchester City kuchukua nafasi ya Pep Guardiola, ingawa yeye mwenyewe alikanusha vikali tetesi hizo. Chelsea, ambao sasa wanatafuta kocha wao wa nne wa kudumu tangu kununuliwa na Todd Boehly na Clearlake Capital mwaka 2022, wanatarajiwa kumtangaza kocha mpya ndani ya siku chache zijazo.




