Elyston Angay awasili Tanzania kwa shoo ya Valentine

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi, Elyston Angay, amewasili nchini Tanzania kwa ajili ya kushiriki katika shoo maalum itakayofanyika usiku wa Siku ya Wapendanao (Valentine Day) katika Ukumbi wa Las Carinyo, uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Ujio wa Elyston Angay unatarajiwa kuipa shoo hiyo mvuto wa kipekee, hasa kwa mashabiki wa muziki wa dansi wa kizazi cha zamani na cha sasa, kutokana na historia yake kubwa katika muziki huo nchini.
Elyston aliingia nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 1990, akijiunga na MK Sound, bendi iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki Asha Baraka, ambapo alijipatia umaarufu na heshima kubwa katika medani ya muziki wa dansi.
Baadaye, kufuatia kuanzishwa kwa Diamond Sound, Elyston Angay aliteuliwa kuwa kiongozi na mpiga gitaa wa bendi hiyo kati ya mwaka 1995 na 1996, kipindi ambacho Diamond Sound ilikuwa ikitumbuiza katika Ukumbi wa Silent Mwenge, moja ya kumbi maarufu za burudani jijini Dar es Salaam wakati huo.
Baada ya kipindi hicho, Elyston Angay aliondoka nchini na kuelekea Zimbabwe, kabla ya kuhamia Afrika Kusini, ambako anaishi kwa sasa akiendelea na shughuli zake za muziki.
Mashabiki wa muziki wa dansi wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani hiyo ya kipekee, itakayomrudisha jukwaani mmoja wa wanamuziki waliowahi kuacha alama kubwa katika historia ya muziki wa dansi Tanzania.




