Edna: Nitaachana na ukocha ndani ya miaka mitano

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Yanga Princess, Edna Lema, ametangaza wazi kuwa huenda akastaafu kazi ya ukocha ndani ya miaka mitano ijayo endapo hatopata nafasi ya kufundisha timu ya wanaume katika Ligi Kuu au Championship kama Kocha Mkuu.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii, Edna amesema kuwa malengo yake makubwa ya sasa ni kupanda ngazi katika taaluma ya ukocha na kupata changamoto mpya nje ya Tanzania, huku akisisitiza kuwa ana kiu ya kujifunza zaidi kupitia vitendo na si nadharia pekee.
“Kama ndani ya hii miaka mitano Mungu akinijalia afya njema, kama sitakuwa nimefundisha timu yoyote ya wanaume ya Championship au Ligi Kuu kama kocha mkuu, basi nitaachana kabisa na kufundisha mpira. Nitafanya kazi nyingine za mpira, lakini si ukocha,” Amesema.
Edna pia ameweka wazi kuwa iwapo hatopata nafasi hiyo hapa nchini, basi yuko tayari kwenda kutafuta changamoto mpya nje ya mipaka ya Tanzania.
“Sina kitu kingine cha kujifunza nikiwa hapa tena. Natakiwa kwenda kufundisha nje ili nijue ugumu wake na urahisi wake. Nikiwa najifunza kukosea ndio kupatia,” aliongeza Edna, akionesha dhamira yake ya kweli ya kutafuta mafanikio zaidi katika kazi ya ukocha.
Kwa muda mrefu, Edna Lema amekuwa miongoni mwa makocha wanawake wachache wanaopambana kupenya katika medani ya mpira wa miguu wa wanaume, jambo ambalo bado ni nadra barani Afrika.