Dube aapa kuwaliza sana Ligi Kuu

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube amesema alipokuwepo sasa atafunga sana.
Straika huyo ameifungia Yanga bao moja katika ushindi wa mabao 4-1, mchezo wa Fainali Ngao ya Jamii uliochezwa jana Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, huku mwenyewe akitamka wazi kuwa, wapinzani kazi wanayo.
“Yanga ina Wachezaji wenye uwezo mkubwa sana ndio maana naamini kuwa, tunaweza kupata idadi kubwa ya mabao. Naamini ninaweza kufunga mabao mengi zaidi ya misimu yote, kikubwa ni kushirikiana kila mchezo tutakaocheza,” alisema staa huyo ambaye alikataa mwenyewe kuichezea Azam akidai haina malengo.
Kabla ya kufunga kwenye mchezo huo, Dube alianza kuonyesha uimara wake kambini nchini Afrika Kusini akitupia kwenye michezo miwili kati ya michezo mitatu Wanajangwani hao waliyocheza kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam.
Mchezo ambao Dube hakufunga kati ya michezo hiyo mitatu ni dhidi ya Ausgburg ya Ujerumani Wanajangwani hao wakilala kwa mabao 2-1, bao la kusawazisha likifungwa na Jean Baleke, lakini mchezo uliofuata dhidi ya TS Galaxy akifunga bao katika ushindi wa 1-0.
Alifunga bao katika mchezo uliofuata wa mwisho dhidi ya Kaizer Chiefs michuano ya Toyota, Wanajangwani hao wakiibuka na ushindi wa mabao 4-0, mengine yakifungwa na Stephane Aziz KI aliyepachika mawili lingine likifungwa na Clement Mzize.
Kudhihirisha kwamba yupo Yanga kikazi zaidi, aliupiga mwingi mbele ya Azam akifunga bao la kwanza, huku akipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa akina Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya na wengine jambo linalomfanya kuamini kwamba atafunga sana