Droo UCL ni leo

MONACO: DROO ya mechi za ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inatarajiwa kupangwa hii leo Agosti 28 baada ya kukamilika kwa idadi ya timu zitakazomenyana kwenye msimu wa pili wa mfumo mpya wa ligi, Droo itakayochezeshwa katika ukumbi wa Grimaldi Forum jijini Monaco nchini Italia.
Timu 36 zimegawanywa katika vyungu vinne mahsusi kwa droo hiyo kulingana na viwango vya klabu. Kila timu itacheza dhidi ya nyingine mbili kutoka kila Chungu na mechi nyumbani na ugenini.
Vyungu vilivyopangwa
Chungu cha 1: Paris St Germain, Manchester City, Real Madrid, Bayern Munich, Liverpool, Inter Milan, Chelsea, Borussia Dortmund na Barcelona.
Chungu cha 2: Arsenal, Bayer Leverkusen, Atletico Madrid, Benfica, Atalanta, Villarreal, Juventus, Eintracht Frankfurt na Club Brugge.
Chungu cha 3: Tottenham Hotspur, PSV Eindhoven, Ajax Amsterdam, Napoli, Sporting CP, Olympiakos, Slavia Prague, Bodo/Glimt, Olympique de Marseille.
Chungu cha 4: FC Copenhagen, AS Monaco, Galatasaray, Union SG, Qarabag, Athletic Bilbao, Newcastle United, Pafos, na Kairat Almaty.
Kwa mara nyingine tena teknolojia itatumika kwenye droo hii ambapo itaanza na chungu cha kwa kwanza mpira mdogo wenye jina la timu utachukuliwa kisha mfumo maalum wa kielektroniki utachagua wapinzani nane, wawili kutoka katika kila chungu huku ikikwepa kuzipa timu wapinzani kutoka nchi yao na zitakuwa na kikomo cha kucheza dhidi ya klabu mbili tu kutoka nchi nyingine.
Mechi za kwanza zimepangwa kuchezwa kuanzia Septemba 16 hadi 18 na fainali Mei 30, 2026 katika uwanja wa Puskas Arena mjini Budapest, Hungary.