Dream team yaanza kwa kishindo michuano ya Taifa Cup

DODOMA: MICHUANO ya Taifa Cup 2025 inaendelea kupamba moto mkoani Dodoma huku timu mbalimbali zikionesha makali yao katika hatua za awali za mashindano hayo ya kitaifa ya mpira wa kikapu.
Katika mchezo wa kuvutia na wa aina yake, Dar es Salaam ‘The Dream team’ iliibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya Mbeya kwa pointi 111 kwa 23. Kikosi cha Dar es Salaam kilitawala mchezo huo kwa kila kipengele, kikionesha uwezo mkubwa wa kiufundi, kasi, na umakini katika kulinda na kushambulia.
Kwa upande wa wanawake, Morogoro waliandika walishinda pointi 58 kwa 51 dhidi ya Tabora. Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa huku pointi zikipatikana kwa juhudi na nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa pande zote mbili, lakini Morogoro waliibuka kidedea kwa tofauti ya pointi saba.
Katika michezo mingine ya wanaume, timu ya Mtwara iliibuka na ushindi wa pointi 68-62 dhidi ya Kigoma. Ushindi huo unaashiria nidhamu na umakini wa timu ya Mtwara hasa katika nusu ya pili ya mchezo ambapo waliongeza kasi na kutawala.
Nao Arusha waliichapa Singida kwanl pointi 68-50, wakionesha ubora mkubwa wa kiuchezaji na ufanisi katika kumalizia mashambulizi yao. Mchezo huo uliwavutia mashabiki wengi waliokusanyika uwanjani kushuhudia vijana wakionesha vipaji vyao.
Mashindano ya Taifa Cup yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza na kuibua vipaji vipya nchini, huku kila mchezo ukiweka alama ya ushindani na mshikamano wa kitaifa.