Dili la Guede kutua Singida Black Stars limefika patamu

DAR ES SALAAM: HUENDA aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Joseph Guede akasajiliwa na Singida Black Stars Stars kuimarisha safu yao ya ushambuliaji wa msimu 2024/25 wa mashindano ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara.
Msemaji wa Singida Black Stars, Hussein Massanza ameiambia Spotileo, kuwa hawajamaliza usajili na ikitokea wanahitaji huduma ya mshambuliaji huyo hawatasita kumsajili kwa kuwa mpaka sasa ni mchezaji huru.
Guede aliyejiunga na Yanga kipindi cha dirisha dogo kwa mkataba wa miezi sita ambao umetamatika na inaelezwa kuwa nyota huyo hatakuwa kwenye mipango ya Yanga kwa msimu ujao na kuhusishwa na Singida Black Stars.
“Usajili unaendelea kila mmoja ameona uwezo wa Guede kama jicho la Kamati la usajili litamuona mshambuliaji huyo basi lolote linaweza kutokea kwa sababu amemaliza mkataba na Yanga ni mchezaji huru,” amesema Massanza.
Ameongeza kuwa wakati kikosi cha timu hiyo kinajiandaa na michuano ya Kagame, usajili unaendelea hadi siku ya mwisho kuimarisha kila eneo ikiwemo ushambuliaji kuleta watu ambao watasaidia timu hiyo kufikia malengo.
Kuhusu kiungo wa kati, Duke Abuya anayehusishwa na Yanga, Massanza amesema nyota huyo amemaliza mkataba wake, kutokuwepo au kuwepo ni suala la kamati ya usajili kushirikiana na benchi la ufundi linaloongozwa na Patrick Aussems.
“Timu inaendelea na maandalizi na kuna baadhi ya wachezaji wataonekana katika Michezo yetu ya Kagame na wengine wapya wataonekana siku yetu maalum ya kutambulisha timu yetu itafanyika Agosti, mwaka huu, Singida,” amesema msemaji wa timu hiyo.