Davido aweka wazi siri ya kufuatiliwa zaidi Afrika

LAGOS: MKALI wa Afrobeats David Adeleke, maarufu Davido, ameweka wazi sababu inayomfanya ashikilie taji la msanii wa Kiafrika anayefuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii.
Akiongea katika mahojiano BET Talks, mwimbaji huyo aliyeshinda tuzo kadhaa alihusisha ufuasi wake mkubwa mtandaoni na uwazi wake, uhalisi, na uhusiano mzuri na mashabiki wake.
“Mimi ndiye msanii wa Kiafrika anayefuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu niko huru na mashabiki wangu,” Davido alisema. “Mwanzoni mwa kazi yangu, nilikuwa muwazi sana. Nilikuwa nafanya vlogs, nikiwaonesha watu maisha yangu. Wasanii wengi wa Nigeria na Afrika huwa na hofu ya kuonesha uhalisi wao.”
“Nadhani kuishi Marekani kulinisaidia sana, pia, kwa sababu akili yangu iko wazi. Sisemi watu wangu ni wajinga… lakini wasanii wengine wanafikiria kupita kiasi,” ameeleza.
Davido amesisitiza kwamba ingawa anafurahia kung’aa na kupendeza inapohitajika, yeye pia ana ujinga wake anaoupenda ikiwemo kupiga picha akiwa na ndala huku akiwa amevaa kaptura akiwa nyumbani kwake kunampa uhuru mno wa kutambulika yeye ni mtu wa kawaida na akidai kwamba hivyo ndiyo inavyotakiwa kuwa kwa wasanii wengine.